Ayatullah Khamenei: Marekani ni adui mkubwa wa utawala wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i79008-ayatullah_khamenei_marekani_ni_adui_mkubwa_wa_utawala_wa_kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo ameashiria watu wanaoitaja kaulimbiu ya "Mauti kwa Marekani" inayotolewa na wananchi wa Iran kuwa ndiyo sababu ya uhasama wa siku zote wa ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Marekani ni adui mkubwa wa utawala wa Kiislamu, kwa sababu utawala huo unatokana na dini na ni dhihirisho la itikadi za kidini za wananchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2022 10:22 UTC
  • Ayatullah Ali Khamenei
    Ayatullah Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo ameashiria watu wanaoitaja kaulimbiu ya "Mauti kwa Marekani" inayotolewa na wananchi wa Iran kuwa ndiyo sababu ya uhasama wa siku zote wa ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Marekani ni adui mkubwa wa utawala wa Kiislamu, kwa sababu utawala huo unatokana na dini na ni dhihirisho la itikadi za kidini za wananchi.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mjumuiko wa matabaka mbalimbali ya wananchi wa Qum kwa mnasaba wa harakati ya wananchi ya Januari 9, 1978 katika mji huo mtakatifu dhidi ya utawala wa zamani wa Shah Pahlavi ambao ulikuwa unapata himaya ya Marekani. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dhihirisho na kielelezo cha Uislamu na utawala wa Umma wa Kiislamu.

Vilevile amegusia mapenzi makubwa ya Waislamu wa madhehebu za Sani katika nchi tofauti kwa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Mahafali kubwa za kumuenzi Shahidi Qasem Soleimani katika nchi za Kiislamu ni mfano wa mapenzi na uungaji mkono wa Umma wa Kiislamu kwa Jamhuri ya Kiislamu kuanzia Asia Mashariki hadi Magharibi mwa Afrika.

Qum

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mazishi ya kihistoria ya Shahidi Qasem Soleimani ni kielelezo cha mlipuko wa hamasa inayotengeneza fursa ya wananchi na kubainisha kuwa: Katika shughuli hiyo, taifa la Iran kwa mara nyingine tena lilionesha waziwazi umoja na utambulisho wake wa kidini na kimapinduzi; na lau mwili huo mtukufu ungepelekwa Syria, Lebanon na Pakistan ungepewa mapokezi makubwa ya mataifa ya Waislamu kama ilivyokuwa nchini Iran na huko Iraq.

Wananchi wa matabaka mbalimbali wa Qum

Ayatullah Khamenei amekitaja kitendo cha kumuua shahidi Kamanda Soleimani kuwa ni mfano wa kuendelea mahesabu mabovu ya Wamarekani na kuongeza kuwa: Magaidi walitaka kumuua Kamanda Soleimani aliyekuwa nembo ya harakati adhimu aliyoiwakilisha, lakini harakati kubwa ya taifa la Iran na watu wa mataifa mengine ya kuonesha mapenzi na uungaji mkono wao kwa jamadari huyo katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuliwa kwake shahidi, ambayo kwa hakika imetokana na nguvu ya Mwenyezi Mungu, imeonesha kwamba, kikokotoo cha Marekani kina dosari na kimeharibika.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja "kutosalimu amri mbele ya adui mwenye kiburi na dhalimu" kuwa ni katika misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Kufanya mazungumzo na kuwasiliana na adui katika baadhi ya vipindi hakuna maana ya kusalimu amri mbele yake; kama ambavyo hatujawahi kusalimu amri na wala hatutasalimu amri."