Abdollahian na Guterres wanabadilishana mawazo kuhusu hali ya Asia Magharibi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Yemen na Afghanistan na mchakato wa mazungumzo ya nyuklia ya Vienna.
Katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amegusia hali ya Yemen na kushadidi mashambulizi dhidi ya makazi ya raia na kusisitiza msimamo wa Iran wa kuunga mkono suluhisho la kisiasa la kukomesha vita nchini Yemen.
Vilevile ameashiria mwenendo wa Umoja wa Mataifa wa kutaka kukomesha mzingiro dhidi ya raia wa Yemen, kusitishwa vita na kuanza mazungumzo ya kisiasa nchini humo na ametoa wito kwa Katibu Mkuu wa UN kuwa nafasi kubwa zaidi katika kukomesha mzingiro huo na kusimamishwa mashambulizi makubwa ya mabomu katika maeneo ya raia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia huko Vienna na kusisitiza azma kubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kufikia makubaliano mazuri haraka iwezekanavyo.
Amir Abdollahian pia amesema, Tehran haina imani kwa watawala wa Ikulu ya White House, na kusisitiza kwamba, kuna haja kwa Magharibi na Marekani kuchukua hatua za kivitendo zinazoweza kuthibitishwa ili kufikia makubaliano ya kudumu na ya kuaminika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepongeza na kukaribisha misimamo dhabiti ya Iran ya kuunga mkono mchakato wa amani, kukomeshwa mashambulizi ya kijeshi, kutilia maanani masuala ya kibinadamu na kuanza mazungumzo ya kisiasa ya kutatua masuala na matatizo ya Yemen.
Antonio Guterres pia amesisitiza haja ya kuendelezwa juhudi za kuunda serikali jumuishi inayoshirikisha makundi na makabila tofauti nchini Afghanistan, pamoja na kutayarishwa mazingira sahihi kwa raia wote wa Afghanistan, hususan wanawake na watoto, kutumia haki zao za binadamu na kupata elimu.