Iran yataka mauaji ya Wayemen yasitishwe mara moja
Ali Asghar Khaji mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Yemen, Hans Grundberg ambapo ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kusitisha vita dhidi ya Yemen.
Mkutano huo wa Khaji na Grundberg ulifanyika Jumamosi kwa njia ya video katika fremu ya azma ya Iran ya kutatua mgogoro wa kibinadamu Yemen.
Kkatika kikao hicho, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Yemen alisisitiza haja ya mzingiro dhidi ya Yemen kuondolewa, vita visitishwe na mazungumzo ya kisiasa yaanze tena katika nchi hiyo.
Kufuatia uungaji mkono wa Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, Saudi Arabia iliivamia kijeshi nchi masikini ya Yemen mnamo Machi 2015 na kuiwekea mzingiro wa pande zote wa nchi kavu, anga na majini. Lengo la vita hivyo lilikuwa ni kuiondoa madaraknai harakati ya Ansarullah lakini Wasaudi wameshindwa kufikia lengo hilo. Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.
Hivi karibuni Shirika la Entesaf la Kupigania Haki za Wanawake na Watoto lenye makao yake nchini Yemen, limesema watoto zaidi ya 300 wa Kiyemen wanaaga dunia kila siku kutokana na utapiamlo wa kiwango cha juu, hali ambayo imesababishwa na vita vya Saudia dhidi ya nchi hiyo.
Hadi hivi sasa uvamizi huo wa Saudia na waitifaki wake umesababisha malaki ya Wayemen kuuawa, wengine wengi kujeruhiwa huku mamilioni ya wengine wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.