Umoja wa Mataifa wapongeza ukarimu wa Iran kwa wakimbizi wa Afghanistan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesifu ukarimu7 wa mataifa mawili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan kutokana na kuwapokea wakimbizi kutoka nchini Afghanistan.
Antonio Guterres sambamba na kuyakumbusha mataifa mengine ya dunia kulisaidia taifa la Afghanistan amesema kinagaubaga kwamba, ukarimu wa Pakistan na Iran siyo jambo la kusahaulika kutokana na mataifa hayo kuwapokea mamilioni ya wakimbizi kutoka Afghanistan na kuwahudumia.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres sanjari na kuthamini na kupongeza ukarimu wa Iran na Pakistan amesema kuwa, “Kwa hakika mimi siwezi kusahau ukarimu wa mataifa kama Iran na Pakistan ambayo yamejitolea na kuwapokea mamilioni ya wakimbizi kutoka nchini Afghanistan.”
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameikumbusha jamii ya kimataifa na kuitaka ilisaidie taifa la Afghanistan ambapo kwa sasa linakabiliwa na matatizo chungu nzima ukiwemo uhaba wa chakula na huduma nyingine muhimu.
Ramiz Alac mtaalamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya chakula anaamini kuwa, takribani theluthi moja ya wakazi milioni 38 wa Afghanistan wanakabiliwa na hali ya dharura na mgogoro wa chakula unaondelea na kwamba, kunahitajika mabilioni ya dola kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo.
Nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na kijamii baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kuidhibiti tena Afghanistan hatua ambayo ilifuatiwa na baadhi ya mataifa wahisani kuikatia misaada na hata kuiwekea vikwazo nchi hiyo.