Amir-Abdollahian: Iran iko tayari kikamilifu kufikia makubaliano mazuri, imara na endelevu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza ulazima wa kuzingatiwa maslahi ya taifa la Iran na mistari myekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akabainisha kwamba, Tehran iko tayari kikamilifu kufikia makubaliano mazuri, imara na endelevu ya nyuklia.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu hapo jana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdurahman Al Thani.
Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Qatar amepongeza mchango chanya wa Iran katika mazungumzo ya Vienna na akatilia mkazo ulazima wa pande zote kufanya juhudi ili kufikia mwafaka.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Abdurahman Al Thani ameeleza pia kuwa, kuna umuhimu wa kufanyika mashauriano ya mara kwa mara baina ya nchi mbili kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kustawishwa uhusiano wa pande mbili na kubadilishana mawazo pia kuhusu masuala yanayopewa umuhimu wa pamoia na Tehran na Doha katika uga wa kikanda na kimataifa.

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian alifanya mazungumzo mengine kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein ambapo alisisitiza tena kuhusu nia ya dhati iliyonayo Iran ya kufikia mwafaka mzuri, imara na endelevu na akaongezea kwa kusema: Marekani inapaswa kuonyesha kivitendo hiyo nia njema inayodai kuwa nayo.
Duru ya nane ya mazungumzo ya nyuklia ya Vienna, iliyoanza Februari 8 mwaka huu katika mji mkuu huo wa Austria, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na vya kinymume cha sheria ilivyowekewa Iran, ilisitishwa kwa mara nyingine tarehe 11 Machi.../