Khatibzadeh: OIC inapaswa kuuzuia utawala wa Kizayuni kujipenyeza katika Ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81708-khatibzadeh_oic_inapaswa_kuuzuia_utawala_wa_kizayuni_kujipenyeza_katika_ulimwengu_wa_kiislamu
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema jumuiya hiyo inapaswa kuzuia kujipenyeza kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Mar 23, 2022 10:03 UTC
  • Khatibzadeh: OIC inapaswa kuuzuia utawala wa Kizayuni kujipenyeza katika Ulimwengu wa Kiislamu

Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema jumuiya hiyo inapaswa kuzuia kujipenyeza kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Saeed Khatibzadeh amesema leo (Jumatano) katika siku ya pili ya Mkutano wa 48 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC mjini Islamabad kwamba, sera ya utawala za Kizayuni wa Israel na muungaji mkono wake mkuu yaani Marekani, ya kupeleka mbele siasa za kikoloni za kuhalalisha kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya utawala huo ghasibu na nchi za Kiislamu imekaribishwa na baadhi ya wanachama wa OIC, na hii ni hatari kwa nchi zinazojali umoja na ustawi wa Umma wa Kiislamu.

Khatibzadeh ameongeza kuwa: "Kukombolewa ardhi yote ya Palestina na kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu kunapaswa kupewa kipaumbele kama kadhia muhimu ya Umma wa Kiislamu."

Khatibzadeh amesema wananchi wa Palestina wanaendelea kuteseka kutokana na kuendelea uvamizi wa kikatili dhidi ya nchi yao na wananyimwa haki za kimsingi za binadamu.

Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu sambamba na kusisitiza msimamo wake wa kudumu wa kupinga vikali hatua yoyote ya mapatano na Israel ili kuendeleza siasa mbovu za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo, inapaswa pia kuchukua hatua madhubuti dhidi ya janga hili la umoja na ustawi wa Umma wa Kiislamu na kuuzuia utawala wa Kizayuni kupenya katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Saeed Khatibzadeh amesema: Iran licha ya kuwaunga mkono kikamilifu wananchi wa Afghanistan, inahimiza utawala wa muda kuunda serikali jumuishi na kutekeleza majukumu yake yanayotambulika kimataifa ikiwemo kuheshimu haki za wanawake na watoto.

Mwakilishi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: Iran inalaani mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria, sambamba na kuunga mkono haja ya kuwadhaminia usalama na ustawi kamili wa wananchi wa Syria.

Amesema: Iran daima imekuwa ikiunga mkono utatuzi wa migogoro na masuala yanayohusiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa njia ya mazungumzo na kutumia njia za amani.

Mkutano wa 48 wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ulianza jana Jumanne mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.

Wawakilishi wa nchi za Kiislamu walinahudhuria katika kikao hicho wanajadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu hususan kuamua namna ya kusaidia juhudi za kupunguza matatizo ya nchi za Kiislamu zilizoathiriwa na mgogoro.