Moqtadai: Ulaya haina chaguo jingine isipokuwa kutekeleza matakwa ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81874-moqtadai_ulaya_haina_chaguo_jingine_isipokuwa_kutekeleza_matakwa_ya_iran
Naibu wa Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitovuka mistari yake myekundu iliyoitangaza wazi na kwamba Ulaya haina njia nyingine isipokuwa kuheshimu na kutekeleza matakwa ya Iran.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Mar 28, 2022 02:49 UTC
  • Moqtadai: Ulaya haina chaguo jingine isipokuwa kutekeleza matakwa ya Iran

Naibu wa Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitovuka mistari yake myekundu iliyoitangaza wazi na kwamba Ulaya haina njia nyingine isipokuwa kuheshimu na kutekeleza matakwa ya Iran.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Abbas Moqtadai akisema hayo wakati akizungumzia safari ya hapa Tehran ya Enrique Mora, Naibu wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kuelewa kuwa kutozingatia na kutilia maana manufaa ya taifa la Iran ni kwa madhara ya madola hayo hayo ya Ulaya.

Amesema, nchi za Ulaya zimeshindwa kuliridhisha taifa la Iran, zimeshirikiana na Marekani katika kutotekeleza ahadi zao ndani ya JCPOA na hivi sasa pia muda unazidi kupita na zimeshindwa kurekebisha misimamo yao.

Abbas Moqtadai

 

Naibu wa Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni wa Bunge la Iran vile vile amesisitiza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kuelewa kuwa, hatua zao za kujichukulia maamuzi kivyao na kutojali manufaa ya taifa la Iran zitazitumbukiza nchi hizo katika mikwamo na matatizo mbalimbali.

Enrique Mora, Naibu wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na ambaye pia ndiye mratibu wa mazungumzo ya Vienna aliwasili mjini Tehran jana Jumapili na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian na Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Iran ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya siasa, Ali Bagheri.