Aprili Mosi; Siku ya kuanza demokrasia ya kidini katika Iran ya Kiislamu
Tarehe 12 Farvardin kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Aprili, ni siku ambayo wananchi wa Iran walishiriki kwa wingi katika kura ya maoni na kuchagua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu utawale humu nchini.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni iliyofanyika miaka 43 iliyopita na ambayo yalitangazwa tarehe Mosi Aprili 1979 yalionesha kuwa asilimia 98 ya walioshiriki kwenye kura hiyo walichagua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu utawale nchini Iran.
Kura hiyo ya maoni ilifanyika katika kipindi cha siku mbili yaani tarehe 30 na 31 Machi 1979 katika kona zote za Iran. Wairani milioni 20 waliokuwa wametimiza masharti ya kupiga kura walishiriki kwenye kura hiyo iliyoitishwa katika kipindi cha siku 50 tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini.
Siku hiyo ni muhimu sana katika kalenda wa Iran na inahesabiwa kuwa ni Siku ya Jamhuri ya Kiislamu. Maadhimisho ya siku hiyo yanafanyika kila mwaka na ni siku rasmi ya mapumziko.
Huo ulikuwa ni uzoefu wa kwanza wa wananchi wa Iran kushiriki kwenye uchaguzi huru ambapo hawakuwahi kupata uzoefu kama huo wakati wa tawala za kiimla na kidikteta za watawala vibaraka waliopinduliwa na wananchi.