Iran: Uzalishaji wa mafuta ghafi umerejea katika kiwango cha kabla ya vikwazo
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kiwango cha uzalishaji wa mafuta ghafi ya taifa hili kimeongezeka na kurejea katika kiwango cha kipindi cha kabla ya vikwazo, ilivyowekewa nchi hii na utawala wa Donald Trump baada ya kuiondoa Marekani kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018.
Javad Owji amesema hayo katika mahojiano na kanali moja ya televisheni hapa nchini na kuongeza kuwa, "Hii leo, tunazalisha mapipa milioni moja na laki nane ya mafuta ghafi kwa siku, kiwango tulichokuwa tukizalisha kabla ya vikwazo."
Amesema Jamhuri ya Kiislamu imeongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta yake ghafi kutokana na mahitaji na ongezeko la masoko mapya ya bidhaa hiyo, huku ikitumia mbinu tofauti ya mikataba ya uuzaji mafuta na kuwategemea wahudumu wake shupavu wenye kuchapa kazi kwa moyo wa kujitolea.
Waziri wa Mafuta wa Iran ameeleza bayana kuwa, kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta ya nchi hii, kutaliletea nguvu taifa hili kiusalama na kiuchumi, na kwamba sekta ya mafuta na gesi ya Iran imeimarika zaidi licha ya vikwazo vya kiwango cha juu mno vya Marekani.

Amegusia juu ya vikwazo vya kiuchumi, kifedha, na kiteknolojia vya maadui dhidi ya Iran na kubainisha kuwa, licha ya vikwazo hivyo, lakini hatua kubwa zimechukuliwa katika kustawisha sekta ya mafuta na gesi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kadhalika Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ongezeko la uzalishaji wa gesi nchini na kueleza kuwa, hatua nzuri zilizochukuliwa na Shirika la Taifa la Gesi la Iran katika msimu uliopita wa baridi kali, zimepelekea kiwango cha uzalishaji gesi asilia katika kampuni ya gesi ya South Pars katika Ghuba ya Uajemi kifikie mita mraba milioni 705 kwa siku.