Iran yakaribisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusimamisha mapigano nchini Yemen
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha mpango wa Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen wa kusimamisha operesheni za kijeshi nchini humo kwa muda wa miezi miwili na kuruhusu kuingia meli znazobeba chakula na mafuta, pamoja na kufunguliwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.
Hans Grundberg, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen alitangaza Ijumaa usiku kwamba Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen na muungano vamizi wa Saudi Arabia wamekubaliana na pendekezo la kusitisha vita kwa miezi miwili, ambako kutaanza kutekelezwa saa saba mchana leo Jumamosi, tarehe 2 Aprili.
Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, mapema leo Jumamosi amesema anatarajia kuwa hatua hii inaweza kuwa utangulizi wa kuondolewa kikamilifu mzingiro na kuanzishwa usitishaji vita wa kudumu ili kupata suluhu la kisiasa la mgogoro wa Yemen.
Akisisitiza mtazamo wa Iran wa kuunga mkono suluhisho la kisiasa na kibinadamu nchini Yemen, Khatibzadeh amesema: "Tunatumai kuwa katika mkesha wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwa kuyapa kipaumbele masuala ya kibinadamu na kuendeleza usitishaji vita, tutashuhudia kuboreshwa kwa hali ya kibinadamu na kubadilishana mateka na mahabusu baina ya pande mbili."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza matumaini yake kuwa hatua hiyo inaweza kufungua njia kwa ajili ya mpango wa kisiasa wa kutatua mgogoro huo.
Mwezi Machi 2015 Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, ilianzisha uvamizi wa kijeshi nchini Yemen na kuizingira nchi hiyo kutokea nchi kavu, baharini na angani.
Maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen wameuawa katika mashambulizi ya Saudia na washirika wake na wengine zaidi ya milioni nne wamelazimika kuwa wakimbizi.