Iran yataka vikwazo vyote dhidi ya wananchi wa Yemen viondolewe haraka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82312-iran_yataka_vikwazo_vyote_dhidi_ya_wananchi_wa_yemen_viondolewe_haraka
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Kuwait kwamba Tehran imepokea vizuri hatua ya kusimamishwa vita nchini Yemen na inaamini kuwa ni jambo la dharura kuondolewa vikwazo vyote ilivyowekewa nchi hiyo ili iwe rahasi kupeleka misaada ya kibinaadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 09, 2022 02:37 UTC
  • Iran yataka vikwazo vyote dhidi ya wananchi wa Yemen viondolewe haraka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Kuwait kwamba Tehran imepokea vizuri hatua ya kusimamishwa vita nchini Yemen na inaamini kuwa ni jambo la dharura kuondolewa vikwazo vyote ilivyowekewa nchi hiyo ili iwe rahasi kupeleka misaada ya kibinaadamu.

Hossein Amir-Abdollahian alifanya mazungumzo hayo ya simu jana Ijumaa na waziri mwenzake wa Kuwait, Sheikh Ahmed Nasser al Sabah na kusema, Tehran inatilia mkazo pia ushirikiano wa kivitendo wa kieneo kwa ajili ya usalama, maendeleo na ustawi wa eneo hili zima.

Hivi karibuni, Hans Grundberg, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen alitangaza kufikiwa makubaliano ya kusimamishwa vita kati ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao yake katika mji mkuu Sana'a na serikali iliyojiuzulu ya nchi hiyo ambayo inashirikiana na wavamizi wa Yemen.

Wakimbizi wa Yemen

Baada ya kutangazwa habari hiyo, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alipongeza ubunifu wa mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa wa kusimamishwa vita kwa muda wa miezi miwili nchini Yemen ambapo imekubaliwa pia kuruhusiwa kuingia meli za misaada ya kibinadamu na kufunguliwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Kuwait wamejadiliana pia mazungumzo ya Vienna kuhusu mradi wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu na udharura wa kuondolewa haraka vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Iran kwa kisingizio cha mradi wake huo wa amani wa nyuklia.