Iran yataka mzingiro dhidi ya Yemen uondolewe kikamilifu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82442-iran_yataka_mzingiro_dhidi_ya_yemen_uondolewe_kikamilifu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza ulamiza wa kuondolewa kikamilifu mzingiro dhidi ya Yemen na kufikiwa mapatano ya kudumu ya usitishwaji vita ili hatimaye mazungumzo ya amani ya Wayemen yaanze.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2022 23:25 UTC
  • Iran yataka mzingiro dhidi ya Yemen uondolewe kikamilifu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza ulamiza wa kuondolewa kikamilifu mzingiro dhidi ya Yemen na kufikiwa mapatano ya kudumu ya usitishwaji vita ili hatimaye mazungumzo ya amani ya Wayemen yaanze.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana mjini Tehran alipokutana na Balozi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen Ibrahim  Mohammad al-Dailami.

Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mapambano ya Wayemen ambao wanakabiliwa na mashambulizi ya muungano vamizi wa kijeshi unoongozwa na Saudia Arabia na kusema ana wasiwasi kuhusu mgogoro ulioko nchini Yemen. Amir-Abdollahian amesema kuna ulazima wa kuondolewa kikamilifu mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini ambao umewekwa Yemen na wavamizi. Ameendelea kusema kuwa baada ya kuondolewa mzingiro, mapatano ya kudumu ya kusitisha vita yanapaswa kufikiwa ili kuandaa mazingira ya mazungumzo ya Wayemen kwa lengo la kuainisha mustakabali wa nchi yao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Wayemen wanapaswa kuainisha hatima yao kwa busara na mapambano.

Kwa upande wake Balozi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen Ibrahim  Mohammad al-Dailami ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwaunga mkono watu wa Yemen. Balozi huyo amemfahamisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusu mchakato wa usitishwaji vita wa muda na matukio mengine nchini Yemen. 

Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen kuanzia mwezi Machi 2015 na kuendelea hadi sasa ambapo umeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha wengine zaidi ya milioni nne wakiwa hawana pa kuishi. 

Uchokozi na uvamzi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen umebomoa na kuharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu na kuisababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa nchi hiyo ya Waislamu.