Iran yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden
-
Saeed Khatibzadeh
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Sweden.
Akijibu kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchini Sweden, Saeed Khatibzadeh amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali kitendo cha mbaguzi wa rangi mwenye misimamo ya kufurutu mipaka cha kuchoma moto Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani katika mji wa Linköping nchini Sweden, jambo ambalo limefanyika kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, chini ya mwamvuli na himaya ya polisi wa Sweden."
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kukaririwa kwa makusudi kitendo hicho cha dharau katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kumezijeruhi hisia za Waislamu nchini Sweden na kote duniani na kuongeza kuwa: Kitendo hiki cha kuvunjia heshima matukufu ya kidini ni mfano wa wazi wa kueneza chuki na kinapingana na uhuru wa kujieleza. Amesisitiza kuwa kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na watu wote wanaoamini fikra ya wanadamu kuishi pamoja kwa amani na mazungumzo baina ya dini mbalimbali.
Khatibzadeh amesema serikali ya Sweden inapaswa kuwajibika katika tukio hilo na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine za Waislamu zinasubiri kuona hatua ya haraka, kali na ya wazi ya serikali ya Sweden ya kukabiliana na wahusika wa vitendo hivyo viovu na kuchukua hatua za wazi na za kivitendo ili kuzuia kutokea tena.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa: "Hatua ya mhalifu huyo na waungaji mkono wake inazidisha udharura wa kuimarishwa zaidi umoja wa Waislamu na nchi za Kiislamu dhidi ya njama za maadui wa Uislamu."