May 23, 2022 07:42 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yalaani kuuawa shahidi Sayyad Khodaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema maadui wa mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena wamedhihirisha dhati ya shari yao kwa ugaidi na kumuua shahidi mmoja kati ya askari wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Idara ya Mahusiano ya Umma ya IRGC jana ilitangaza kuwa mmoja wa askari wake ambaye ni Mlinzi wa Haram ameuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi mjini Tehran Jumapili jioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya IRGC, askari mwenye kuheshimika mlinzi wa Haram Kanali Hassan Sayyad Khodaei aliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya wapinga Mapinduzi ya Kiislamu na maajenti wa madola ya kiistikbari duniani.

Katika taarifa Jumapili usiku, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alituma salamu za pongezi na rambimbi  kwa familia ya Shahidi Sayyad Khodaie.

Aidha amelaani vikali oparesheni ya kigaidi iliyopelekea kuuawa shahidi Kanali Sayyad Khodaei na kusema jinai hii dhidi ya binadamu imetekelezwa na uistikbari wa kimataifa. Hali kadhalika amebainisha masikitiko yake kuwa nchi za Magharibi zinazodai kukabiliana na ugaidi zimenyamazia kimya na kuunga mkono jinai hiyo.

Shahidi Hassan Sayyad Khodaei akiwa ndani ya gari lake baada ya kupigwa risasi

Amesema katika kipindi cha miongo minne Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mhanga wa ugaidi na kuongeza kuwa magaidi wana dhana batili kuwa vitendo vyao vitapelekea taifa adhimu la Iran lishindwe kufikia malengo yake ya juu na kusitisha mchakato wa izza na heshima wa watu wa nchi hii lakini wameghafilika kwani hawafahamu kuwa damu ya mashahidi ndiyo inayodhamini kubakia na kufika daraja la juu taifa hili.

 

Tags