Iran yawawekea vikwazo Wamarekani wanaounga mkono magaidi wa MKO
(last modified Sun, 17 Jul 2022 03:35:18 GMT )
Jul 17, 2022 03:35 UTC
  • Iran yawawekea vikwazo Wamarekani wanaounga mkono magaidi wa MKO

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza orodha mpya ya maafisa wa sasa na wa zamani wa serikali ya Marekani ambao kwa makusudi wamekuwa wakiunga mkono kundi la kigaidi la MKO lililo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika taarifa ya Jumamosi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema imewawekea vikwazo Wamarekani 61 kwa mujibu wa sheria ya Iran yenye anwani ya: “Kukabiliana na Ukiukaji wa Haki za Binadamu, Chokochoko na Vitendo vya Kigaidi vya Marekani katika Eneo”.

Sheria hii ilipitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) mnamo Agosti 2017.

Kati ya wale ambao Iran imewawekea vikwazo ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo na mshauri wa zamani wa usalama wa taifa katika Ikulu ya White House John Bolton ambao wote  wamewahi kushiriki rasmi katika vikao vya kundi la kigaidi la MKO. Aidha wengine walio katika orodha hiyo ya vikwazo ni Seneta Ted Cruz na Seneta Bob Mendez.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema maafisa hao waliotajwa ni waungaji mkono wa kundi la MKO kupitia kushiriki katika vikao vya kundi hilo na kukiri kuhusu vitendo vyao vya kigaidi sambamba na kuunga mkono kundi hilo kipropaganda na kisiasa.

Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kundi la MKO limeandaa na kutekeleza idadi kubwa ya hujuma za kigaidi kwa miongo kadhaa sasa ambapo raia wasiopungua 17,000 wasio na hatia, hasa wanawake na watoto wameuawa.

Pamoja na kuwa ni wazi kuwa MKO ni kundi lenye utambulisho wa kigaidi na  limetenda jinai za kigaidi, lakini Marekani inaendelea kuunga mkono kundi hili na hivyo inaendeleza sera zake za unafiki na undumakuwili kuhusu ugaidi.

Taarifa hiyo imesema Iran inafungamana na majukumu yake ya kimataifa ya kukabiliana na ugaidi na kusema hatua ya Marekani ya kuunga mkono kundi la kigaidi la MKO ni kinyume cha majukumu yake ya kimataifa.