IRGC: Wakati wa Marekani kuweko Asia Magharibi umefikia tamati
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema wakati umefika wa kuondoka Marekani katika eneo la Asia Magharibi kutokana na kupoteza kwake udhibiti na ushawishi katika eneo hili.
Brigedia Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH amesema hayo hapa Tehran katika marasimu ya kuwakumbuka na kuwaenzi Mashahidi wa Haram Tukufu na kusisitiza kuwa, Washington imepoteza dira, na haiwezi tena kutumia stratajia yake ya mashinikizo ya kiwango cha juu.
Kamanda Salami amefichua kuwa, Lebanon ina makombora ya balestiki zaidi ya 100,000, na ambayo yako tayari kuunyeshea utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amefafanua zaidi kwa kusema: Huko Lebanon, kuna makumi ya maelfu ya makombora, au hata zaidi ya laki moja, ambayo yako tayari kuvurumishwa kuelekea Israel na kuugeuza jahanamu utawala wa Kizayuni.
Brigedia Jenerali Salami amesema Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inaweza kuipigisha magoti Israel kwa mara nyingine, kupitia operesheni zinazofanana za zile za huko nyuma za Fat'hul Mubin, Baitul Muqaddas na Khaibar.
Salami ameeleza bayana kuwa, "Iran imefanikiwa kuvishinda vikwazo dhidi ya taifa hili, na changamoto zinazoshuhudiwa hivi sasa hazina uhusiano wowote na vikwazo, na zinaweza kupatiwa ufumbuzi."
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislami imejiandaa barabara kukabiliana na kutoa vipigo vikali dhidi ya maadui, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kiulinzi ukiwemo uwezo wa manowari za kisasa.