Qalibaf: Iran haina imani na Marekani, haitasalimu amri kuhusu haki zake
-
Mkuu wa majeshi ya Pakistan Asim Munir, na Spika wa Bunge la Iran, Muhammad Qalibaf
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema kuwa Iran haina imani yoyote na Marekani na kwamba haitarudi nyuma kamwe katika kutetea haki zake za kitaifa wakati wa mazungumzo na Marekani yanayolenga kuhitimisha vita katika eneo lote la Asia Magharibi.
Qalibaf ameyasema hayo katika mkutano wa Jumamosi na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Field Marshal Asim Munir, ambaye aliwasili Tehran usiku wa Ijumaa kwa ajili ya kubadilishana mawazo na maafisa wa ngazi za juu wa Iran kuhusu matukio ya hivi karibuni ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani yanayopatanishwa na Pakistan.
Amesema, “Hatutarudi nyuma katika haki za taifa letu na nchi yetu, hasa dhidi ya upande ambao hauna uaminifu hata kidogo na ambao hatuna imani nao.”
Qalibaf, ambaye ndiye kiongozi wa timu ya mazungumzo ya Iran, aligusia hatua za kijasiri na madhubuti za ulinzi wa kujitetea za Iran katika medani ya vita, akiongeza kuwa nchi hiyo itafanya kazi kwa hekima na nguvu katika nyanja ya kidiplomasia ili kufanikisha haki zake halali na kulinda maslahi ya taifa.
Alilaumu Marekani kwa kuanzisha vita wakati mazungumzo ya nchi mbili yakiwa yanaendelea, na sasa inataka mazungumzo ili kuvimaliza.
Spika huyo wa Bunge la Iran aliongeza: “Tulikuwa kwenye usitishaji wa mapigano mliopatanisha nyinyi [Pakistan], wakati Marekani ilivunja ahadi yake, ikaweka mzingiro wa kijeshi baharini, na sasa inatafuta njia ya kuondoa mzingiro huo.”
Qalibaf alijibu tetesi kuhusu uwezekano wa kuanzishwa tena kwa uchokozi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akibainisha kuwa Vikosi vya Wanajeshi wa Iran vimetumia kipindi cha usitishaji wa mapigano kujijenga upya.
Alionya kuwa, “Ikiwa [Rais wa Marekani Donald] Trump atafanya upumbavu na kuanzisha tena vita, hakika vitakuwa na madhara makubwa na machungu zaidi kwa Marekani kuliko siku ya kwanza ya vita.”
Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, kwa upande wake, alisema amefurahishwa kuona kuwa Iran inaongozwa na watu wenye busara na wenye mtazamo mpana.