Velayati: China ni muitifaki wa Kiistratijia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, China ni muitifaki wa kiistratijia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Dk Ali Akbar Velayati amesema hayo wakati alipoonana na balozi wa China hapa mjini Tehran, Chang Hua, na kuzungumza naye umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili na pia masuala ya kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Velayati ametilia mkazo wajibu wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa kiistratijia wa Iran na China na kusisitiza kuwa, hivi sasa China inafuatilia miradi yake ya mawasiliano, usafirishaji na uchukuzi hasa kuwa na barabara kuu inayounganisha maeneo tofauti duniani. Iran nayo iko kwenye eneo muhimu sana la kiistratijia na imepiga hatua kubwa katika masuala ya uchukuzi na usafirishaji na mambo hayo yanazidi kutia nguvu udharura wa uhusiano wa kiistratijia baina ya Tehran na Beijing.
Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa vile vile amesema, uhusiano wa Iran, China na Russia katika nyuga tofauti una taathira muhimu na za kudumu.
Kwa upande wake, balozi wa China hapa mjini Tehran ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa msimamo wake wa kuweko China moja na kutilia mkazo kwake uhusiano baina yake na Beijing akisisitiza kuwa, ushirikiano huo inabidi ufuatiliwe kwa uzito mkubwa zaidi kuliko hata hivi sasa.
Chang Hua ameongeza kuwa, uhusiano wa Iran na China umesimama juu ya misingi ya kuheshimiana na kwamba viongozi wa nchi hizi mbili wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha uhusiano huo unazidi kuwa imara.