Iran yaitaka Marekani kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa, iwaachilie Wairani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87148-iran_yaitaka_marekani_kutekeleza_makubaliano_ya_kubadilishana_wafungwa_iwaachilie_wairani
Iran imeelezea utayari wake wa utekelezaji wa haraka wa makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Marekani huku ikiitaka Washington kuwaachia huru Wairani waliofungwa nchini Marekani bila ya kulifungamanisha suala hilo na masuala yasiyo na umuhimu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2022 03:08 UTC
  • Iran yaitaka Marekani kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa, iwaachilie Wairani

Iran imeelezea utayari wake wa utekelezaji wa haraka wa makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Marekani huku ikiitaka Washington kuwaachia huru Wairani waliofungwa nchini Marekani bila ya kulifungamanisha suala hilo na masuala yasiyo na umuhimu.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kan’ani alithibitisha dhamira na irada ya Tehran ya kutekeleza makubaliano kuhusu suala la wafungwa, na kuitaka Marekani kutimiza ahadi zake kuliko "kufanya maonyesho ya tamthilia".

"Jamhuri ya Kiislamu, kupitia njia mbalimbali, imetangaza mara kwa mara utayari wake kwa upande wa Marekani kushughulikia suala la wafungwa bila ya kulifungamanisha na JCPOA," msemaji huyo amesisitiza, akiashiria mapatano ya kimataifa ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Ameitaka Marekani kuwaachilia raia wa Iran waliofungwa jela bila masharti yoyote.

"Tuko tayari kuwezesha ukombozi na kurejea kwa haraka Wairani wasio na hatia, ambao wameangukia katika dhulma [inayofanywa] ya taasisi ya kisheria ya Marekani kwa msingi wa shutuma zisizo na msingi za  kukiuka vikwazo vya kidhalimu na haramu vya Marekani," Kan' ani ameongeza.

Makubaliano hayo yalifikiwa mjini Vienna kando ya mazungumzo kuhusu mkataba wa nyuklia wa JCPOA wa mwaka  2015 na madola sita makubwa duniani.

Tehran mara kwa mara imesema iko tayari kwa mabadilishano ya wafungwa na Marekani kwa kuzingatia makubaliano na bila ya kutegemea mapatano ya nyuklia JCPOA, ambayo Marekani ilichukua hatua ya kujiiondoa kwa upande mmoja mwezi Mei 2018 licha ya Iran kuyatekeleza kikamilifu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken

Matamshi hayo ya Kan’ani yamekuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken na mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu Iran, Robert Malley, kuishutumu Iran kuwa imewaweka kizuizini Wamarekani na kuwatumia kwa “manufaa ya kisiasa.”

Akijibu matamshi hayo yaliyojaa uhasama, Kan’ani ameikosoa Marekani kwa kufanya “michezo ya maonyesho” dhidi ya Iran badala ya kuchukua hatua za kivitendo katika kuondoa vikwazo vilivyoko katika njia ya kubadilishana wafungwa kati ya nchi hizo mbili.

"Inashangaza kwamba Marekani, badala ya kuchukua hatua na kuondoa vikwazo katika uwanja huu, inafanya tu michezo ya kuigiza dhidi ya Iran," amesema.

Hii si mara ya kwanza kwa Jamhuri ya Kiislamu kuikosoa Marekani kwa kudharau makubaliano ya kubadilishana wafungwa.

Iran mara kwa mara imekuwa ikiitaka Washington kuwaachilia huru raia wa Iran ambao wamechukuliwa mateka kwa tuhuma zisizo na msingi za kukiuka vikwazo vya Marekani, ikiilaumu Marekani kwa kulifungamanisha suala la kibinadamu na kufufuliwa mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015.