Iran: Tumeshakabidhi mitazamo yetu kwa mpatanishi kuhusu mazungumzo ya nyuklia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu usiku wa kuamkia leo Ijumaa imekabidhi mitazamo yake kuhusu majibu ya Marekani juu ya muswada wa makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kuhusiana na kuondolewa vikwazo Iran na amesisitiza kuwa, mitazamo hiyo ya Tehran ni ya maana, ya kimsingi na yenye lengo la kufikisha mwisho mazungumzo hayo.
Nasser Kan'ani ametoa taarifa hiyo mapema leo Ijumaa na kuongeza kuwa, baada ya kupokea majibu ya Marekani, timu ya wataalamu ya Jamhuri ya Kiislamu imekaa na kuchunguza kwa kina majibu hayo na hatimaye majibu ya Iran yamekabidhiwa kwa Enrique Mora, mpatanishi wa Umoja wa Ulaya usiku ya kuamkia leo Ijumaa.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ameongeza kuwa, majibu ya Iran yametolewa kwa nia njema, kwa kuzingatia pande zote na kwa lengo la kuondoa vizuizi vyote kwani shabaha ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuona mazungumzo hayo yanafikia natija inayotakiwa.
Awamu mpya ya mazungumzo ya Vienna ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa Iran vikwazo vya kidhalimu, ilifanyika tarehe 4 hadi 8 mwezi ulioisha wa Agosti na kujadiliwa mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na Enrique Mora, mpatanishi wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo hayo.
Takriban nchi zote zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya Vienna zinataka kumalizwa na kufikia natija mazungumzo hayo lakini kinachosubiriwa ni maamuzi ya kisiasa ya Marekani kuhusu maudhui kadhaa muhimu na za kimsingi zilizobakia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni nchi inayoheshimu ahadi zake, mara zote imekuwa ikisisitiza kuwa, Marekani ndiyo iliyojitoa bila ya sababu kwenye mapatano ya JCPOA na ni Washington ndiyo inayopaswa kuiondolea vikwazo Iran ambavyo imeviweka kidhulma kinyume kabisa na makubaliano hayo ya kimataifa.