Iran yaanza kuadhimisha Wiki ya Kujihami Kutakatifu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i88444-iran_yaanza_kuadhimisha_wiki_ya_kujihami_kutakatifu
Maadhimisho ya miaka 42 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran yameanza leo asubuhi katika jiji la Tehran na miji mingine ya taifa hili.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Sep 22, 2022 04:17 UTC
  • Iran yaanza kuadhimisha Wiki ya Kujihami Kutakatifu

Maadhimisho ya miaka 42 ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran yameanza leo asubuhi katika jiji la Tehran na miji mingine ya taifa hili.

Maadhimisho haya yameanza kwa mbwembwe za aina yake, ambapo mapema leo asubuhi vikosi tofauti vya Jeshi la Iran vimepiga magwaride hapa jijini Tehran na katika miji mingine ya Iran.

Mjini Tehran maadhimisho haya yanafanyika jirani na haram ya Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo viongozi wa serikali na makamanda mbalimbali wa ngazi za juu wa jeshi wanashiriki katika maadhimisho haya muhimu katika historia ya Iran.

 

Katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 31 Shahrivar inayosadifiana na tarehe 22 Septemba ni siku vilipoanza vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam dhidi ya Iran, ambapo huanza maadhimisho yaliyopewa jina la Wiki ya Kujihami Kutakatifu.

Itakumbukwa kuwa katika vita vya miaka minane (1980-1988) dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jeshi la utawala wa Baathi wa Saddam liliungwa mkono kwa hali na mali na madola ya kiistikbari na kupatiwa misaada chungu nzima na nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi.

Hata hivyo licha ya mbinyo na vizuizi vya kila upande, Iran iliweza kwa azma thabiti kusimama imara na kukabiliana na ubabe na utumiaji mabavu wa madola makubwa ya dunia yaliyokuwa yakiuunga mkono utawala vamizi wa dikteta Saddam.