Abdollahian asisitiza kupanua ushirikiano kati ya Iran na Pakistan
(last modified Wed, 19 Oct 2022 08:08:07 GMT )
Oct 19, 2022 08:08 UTC
  • Abdollahian asisitiza kupanua ushirikiano kati ya Iran na Pakistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa uhusiano wa Tehran na Islamabd uko katika hali nzuri na kusisitiza juu ya kupanuliwa ushirikiano kati ya Iran na Pakistan katika nyanja zote khususan katika suala la usalama.

Muhammad Sadeq Khan Mjumbe Maalumu wa Waziri Mkuu wa Pakistan katika masuala ya Afghanistan ambaye alikuwa ziarani hapa nchini kufanya mashauriano kuhusu matukio ya Afghanistan jana alikutana na kufanya mazungumzo na Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.  

Katika mazungumzo hayo, Amir Abdollahian ameleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa usalama wa Pakistan ni usalama wake na akasema: Tehran iko tayari kushirikiana na Pakistan ili kuboresha hali ya usalama katika eneo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria uwepo wa raia wa Afghanistan zaidi ya milioni nne na nusu hapa nchini. Amesema, raia zaidi ya milioni moja na nusu miongoni mwao wamewasili Iran baada ya matukio ya mwaka jana na kushika madaraka kundi la Taliban, na kuunga mkono kupatikana amani na uthabiti huko Afghanistan ambako kunapelekea kurejea makwao wakimbizi. Abdollahian amesisitiza pia kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia uwezo wake wote ili kurejesha amani na utulivu huko Afghanistan na kwa ajili ya ustawi wa watu wa nchi hiyo.  

Wakimbizi wa Kiafghani nchini Iran 

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuendesha mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi jirani na Afghanistan. 

Katika mazungumzo hayo, Sadeq Khan Mjumbe Maalumu wa Waziri Mkuu wa Pakistan pia amebainisha wazi mitazamo ya Pakistan kuhusu matukio ya karibuni huko Afghanistan na hali ya mambo ya nchi hiyo ambayo inapelekea kuungua kiwango cha  maisha ya wananchi wa Afghanistan kutokana na sababu za ndani na mashinikizo kutoka nje na kusisitiza kuhusu umuhimu wa nafasi athirifu ya nchi za ukanda huu na jirani na Afghanistan hasa nchi mbili za Iran na Pakistan. 

Mjumbe Maalumu wa Waziri Mkuu wa Pakistan katika masuala ya Afghanistan ameashiria mashauriano chanya kati yake na viongozi wa Iran kuhusu Afghanistan na usalama wa kikanda na kusisitiza kuwa nchi mbili za Iran na Pakistan ndizo zilizoathirika pakubwa kutokana na matukio ya Afganistan kama wimbi kubwa la wakimbizi, kuzorota kwa hali ya maisha ya watu wa nchi hiyo na kuongezeka ukosefu wa usalama na kushtadi kwa biashara ya madawa ya kulevya.

Ameongeza kuwa, ushirikiano wa Iran na Pakistan unaweza kusaidia wananchi wa Afghanistan na kupunguza sana taathira haribifu za hali hiyo tajwa kwa wananchi wa Afghanistan.