Amir Abdollahian: Israel ina matatizo chungu nzima ya kiuchumi na kisiasa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Palestina kwamba utawala wa Kizayuni hivi sasa una matatizo chungu nzima ya kiuchumi na kisiasa.
Omar Awadallah, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Palestina, jana Jumamosi alionana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian pembeni mwa kikao cha Waratibu wa Kitaifa wa Kundi la Marafiki wa Ulinzi wa Hati ya Umoja wa Mataifa hapa mjini Tehran.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia kadhia ya Palestina na vitendo viharibifu vya utawala wa Kizayuni akisisitiza kuwa hayo ni katika mambo muhimu sana ya kujadiliwa na kusisitiza kuwa, kikao hicho cha Tehran kimelipa umuhimu mkubwa suala hilo na limeingizwa kwenye taarifa ya mwisho ya kikao hicho.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Palestina ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada yake kwa wananchi wa Palestina.
Naye Mohamed Lashtar, Mshauri wa Rais wa Nicaragua katika masuala ya Kiarabu na Kiafrika jana alionana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pambizoni mwa kikao hicho.
Balozi Lashtar ametumia fursa ya mazungumzo yake hayo na Hossein Amir-Abdollahian kushukuru ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuitisha kikao hicho cha ngazi za juu cha kulindwa hati ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, Nicaragua ina hamu ya kuimarisha uhusiano wake na Tehran katika nyuga zote.