Iran yaionya Ujerumani: Jibu letu kwa uingiliaji wenu litakuwa zito
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i90346-iran_yaionya_ujerumani_jibu_letu_kwa_uingiliaji_wenu_litakuwa_zito
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali matamshi ya uingiliaji na ya kichochezi yaliyotolewa na mwenzake wa Ujerumani na kuonya kuwa, Tehran itatoa jibu lenye mlingano na madhubuti kwa misimamo hiyo ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hii.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2022 07:37 UTC
  • Iran yaionya Ujerumani: Jibu letu kwa uingiliaji wenu litakuwa zito

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali matamshi ya uingiliaji na ya kichochezi yaliyotolewa na mwenzake wa Ujerumani na kuonya kuwa, Tehran itatoa jibu lenye mlingano na madhubuti kwa misimamo hiyo ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hii.

Hossein Amir-Abdollahian ametoa indhari hiyo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter leo Alkhamisi, kujibu bwabwaja za Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock.

Amir-Abdollahian ametahadharisha kuwa, matamshi ya waziri huyo wa Ujerumani ya kuunga mkono na kushajiisha fujo na ghasia humu nchini yatakuwa na taathira hasi kwa uhusiano mkongwe wa nchi mbili hizi.

Waziri Abdollahian ameitaja kauli hiyo ya mwenzake wa Ujerumani kuwa ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya nchi hii, isiyo ya kidiplomasia na inayoashiria ukosefu wa hekima.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Ujerumani inapaswa kuchagua ama njia ya mazungumzo kwa ajili ya kutafutia ufumbuzi changamoto zilizoko baina ya pande mbili, au makabiliano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock

Jana Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alitangaza kuunga mkono fujo nchini Iran, na kusema kuwa Umoja wa Ulaya umeazimia kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu wiki ijayo.

Nchi za Magharibi zimeteka nyara maandamano yaliyoanza katikati ya mwezi Septemba mwaka huu hapa nchini, kulalamikia kifo cha mwanamke wa Kiirani, Mahsa Amini.

Wamagharibi wametumia kifo hicho kama kisingizio cha kuchochea na kukoleza moto wa ghasia za umwagaji damu na uharibifu wa mali za umma hapa Iran, mbali na kutaka kuligawa na kulishinikiza zaidi taifa hili.