Baqeri: Marekani imeshindwa kuifanya dunia ifuate amri zake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91286-baqeri_marekani_imeshindwa_kuifanya_dunia_ifuate_amri_zake
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amesema Wamarekani wanatambua wazi kuwa wamefeli katika juhudi zao za kuunda dunia yenye kufuata sera, amri na mienendo ya Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2022 00:13 UTC
  • Baqeri: Marekani imeshindwa kuifanya dunia ifuate amri zake

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amesema Wamarekani wanatambua wazi kuwa wamefeli katika juhudi zao za kuunda dunia yenye kufuata sera, amri na mienendo ya Washington.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Kamanda wa Komandi Kuu ya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hayo jana jioni hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Russia anayesimamia masuala ya kimataifa, Kanali Jenerali Alexander Fomin.

Meja Jenerali Baqeri amesisitiza kuwa, Wamarekani hii leo wanakiri waziwazi kuwa njama zao za kuunda dunia yenye muelekeo mmoja zimegonga mwamba.

Kadhalika amesisitizia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa wa Tehran na Moscow katika fremu ya kufikia malengo na maslahi ya pande mbili, sambamba na kuimarisha amani, uthabiti na usalama wa eneo.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran amebainisha kuwa, kupambana na vitisho vya pamoja vya mataifa haya mawili, na kushirikiana katika nyuga zenye masalahi ya pande mbili kunahitaji mashauriano ya mara kwa mara baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Russia.

Kuimarika ushirikiano wa kijeshi wa Iran na Russia

Jenerali Baqeri amesema ushirikiano wa nchi mbili hizi ulifanikiwa na kuzaa matunda katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi nchini Syria na kuongeza kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu ingali inahitaji uungaji mkono wa Tehran na Moscow.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Russia anayesimamia masuala ya kimataifa, Kanali Jenerali Alexander Fomin aliwasili hapa Iran jana Jumamosi, kuja kushiriki mkutano wa nne wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kijeshi hapa Tehran.