Utafiti: Waswahili wana asili ya Kiajemi; nusu ya mababu zao ni Wairani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95770-utafiti_waswahili_wana_asili_ya_kiajemi_nusu_ya_mababu_zao_ni_wairani
Utafiti wa chembe chembe za vinasaba unaonyesha kuwa, Waswahili wa Ukanda wa Pwani Afrika Mashariki wana asili ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2023 03:28 UTC
  • Utafiti: Waswahili wana asili ya Kiajemi; nusu ya mababu zao ni Wairani

Utafiti wa chembe chembe za vinasaba unaonyesha kuwa, Waswahili wa Ukanda wa Pwani Afrika Mashariki wana asili ya Iran.

Utafiti huo uliofanywa kutoka kwa watu 80 waliozikwa katika karne za nyuma katika miji ya uswahili pwani ya Afrika Mashariki umefichua kwamba watu hao walikuwa na asili ya Kiafrika na kutoka Asia.

Utafiti huo wa wataalamu wa kimataifa uliochapishwa katika jarida la sayansi la Nature unaeleza kuwa wanawake wa Kiafrika walizaa na wanaume kutoka barani Asia angalau miaka 1000 iliyopita katika sehemu tofuati pwani ya Afrika Mashariki.

Baadhi ya watu wanaoishi katika pwani ya Afrika Mashariki wanajitambulisha kama Waswahili, licha ya kwamba utambulisho huu huambatana na anakotokea mtu, au ukoo wake.

 

Katika kutathmini asili ya Mswahili - Watafiti wa kimataifa wanaeleza kwamba kuanzia mwaka 1000 baada ya kuzaliwa kwa Yesu, nusu ya chembechembe za vina saba vya watu waliokuwepo iligawanyika kwa 90% kutoka Uajemi na 10% kutoka India. Nusu ya pili ya DNA ikitokana na wanawake wa Kiafrika.

Utafiti huo wa DNA umebaini kwamba kulikuwa na muingiliano baina ya wanaume wa Kiajemi na wanawake wa Kiafrika. Na tangamano hili watafiti hao wanaeleza huenda ulitokana na kwamba wanaume wa Kiajemi walioa katika familia walizofanya nao biasharana kujichanganya na jamii hizo katika kufanikisha biashara zao. Uafiti huo uliochapishwa katika jarida la Sayansi la Nature Journal unaeleza kwamba baada ya mwaka 1500 baada ya kuzaliwa Issa kiasi cha asili hiyo ya Uajemi ilibadilika na kuonyesha Uarabu.