Jun 16, 2023 11:44 UTC
  • Castro asisitiza kuwa zama za maamuzi ya upande mmoja duniani zimeyoyoma na kumalizika

Rais wa zamani wa Cuba amesisitiza kwamba zama za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja duniani zimeyoyoma na kwamba sasa dunia inaelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa.

Raul Castro ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi aliyekuwa safarini nchini Cuba. Amepongeza mapambano ya kimapinduzi ya taifa la Iran na misimamo yake katika kipindi chote cha miaka 44 iliyopita dhidi ya dhulma na ubeberu wa kimataifa na kusema: Hivi sasa enzi za mfumo wa kambi moja zimepitwa na wakati na dunia imo katika kipindi cha kuelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa."

Kwa upande wake, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika mazungumzo yake na Raul Castro kwamba uhusiano wa kisiasa kati ya Tehran na Havana uko katika kiwango cha juu kabisa tangu kuanza kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo ya Rais Ebrahim Raisi na Raul Castro

Sayyid Ebrahim Raisi amesifu subira, msimamo imara na moyo wa kupigania uhuru wa serikali na watu wa Cuba dhidi ya vikwazo visivyo vya haki na vya upande mmoja vya Marekani na amelaani vikwazo vya miongo 6 na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na wale wanaodai kutetea haki za binadamu dhidi ya taifa la Cuba.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza ulazima wa kuweko umoja na mitazamano ya aina moja baina ya nchi zenye mielekkeo sawa kwa ajili ya kukabiliana na ubeberu wa kimataifa hasa kutokana na matukio ya hivi karibuni katika uga wa kimataifa na mwenendo wa sasa wa kuelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa duniani.

Sayyid Raisi ameondoka Havana, mji mkuu wa Cuba kurejea Iran, baada ya kukamilisha safari yake ya kuzitembelea nchi za Venezuela, Nicaragua na Cuba katika eneo hilo la Amerika ya Latini.

Tags