Jun 17, 2023 11:08 UTC
  • Reuters: Mauzo ya mafuta ya Iran nje ya nchi yameweka rekodi

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, ununuzi wa mafuta kutoka Iran mwaka huu 2023 umeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Duru za kuaminika zimeiambia Reuters kuwa, mauzo ya mafuta ghafi ya Iran nje ya nchi mwezi uliopita wa Mei yalipindukia mapipa milioni 3 kwa siku. 

Kiwango hicho kinalandana na kilichotolewa hivi karibuni na Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC), na hakijawahi kushuhudiwa tokea mwaka 2018. 

Nalo shirika la takwimu la Kpler limesema kuwa, Iran iliuza nje ya nchi mapipa milioni 1.5 ya mafuta ghafi mwezi Mei, 2023, kiwango cha juu zaidi kuwahi kusajiliwa baada ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018.

Haya yanajiri siku chache baada ya Kituo cha Takwimu cha Ulaya (Eurostat) kutoa takwimu mpya zinazoonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2018, Ujerumani imeagiza shehena kubwa ya mafuta au bidhaa za petroli kutoka Iran licha ya vikwazo vya Marekani.

Kiwanda cha mafuta cha Iran

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa, mwezi Machi mwaka huu, Ujerumani iliagiza tani 69,737 za mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran. Bulgaria, ikiwa mwanachama mwingine wa Umoja wa Ulaya, pia imeagiza tani 147 za mafuta ghafi au bidhaa za mafuta kutoka Iran katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Wanachama wawili wa Umoja wa Ulaya wameagiza mafuta ghafi au bidhaa za petroli kutoka Iran katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kinyume na sera ya Marekani ya vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran. Nchi za Ulaya hivi sasa zinasumbuliwa na mgogoro mkubwa wa nishati kutokana na vita vya Ukraine.

 

Tags