Aug 03, 2023 11:08 UTC
  • Utulivu tete katika kambi ya Ain Al-Hilweh kufuatia matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah

 Utulivu wa kiwango fulani umerejea katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya   Ain Al-Hilweh nchini Lebanon kufuatia matamshi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrallah, ya kusisitizia ulazima wa kusitishwa mapigano katika kambi hiyo.

Mapigano makali ya utumiaji silaha yalianza Ijumaamosi usiku katika kambi ya Ain Al-Hilweh. Kambi hiyo, ambayo ni maalumu kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina, iko katika eneo la Saida kusini mwa Lebanon.

Jaribio lililofeli la mauaji ya Mahmoud Khalil maarufu kwa lakabu ya Abu Qatadah, mmoja wa makamanda wa kundi la Wapalestina liitwalo Asabatul-Ansar katika kambi hiyo ya Ain Al-Hilweh, ndilo lililokuwa chanzo cha kuzuka mapigano hayo. Kamanda huyo wa kiusalama alijeruhiwa, lakini mkimbizi mmoja wa Kipalestina ambaye ni mwanachama wa kundi la Al-Shabaab al-Muslim aliuawa na watu wengine sita, wakiwemo watoto wadogo wawili, walijeruhiwa.

Mapigano yalishtadi na kupamba moto siku ya Ijumaapili, baada ya mauaji ya Abu Ashraf al-Armoushi, kamanda wa usalama wa taifa wa Palestina na mwanachama mwandamizi wa harakati ya Fat-h katika mji huo wa Saida. Siku ya Ijumaatatu na Ijumaanne, mapigano hayo yanayotia shaka, yaliendelea katika kambi hiyo kwa kufyatuliwa maroketi na kuhanikiza milio ya risasi na magurunedi ya RPG. Duru za habari ziliripoti kushiriki wanamgambo wenye silaha wa kundi lenye misimamo ya kufurutu mpaka la Jundu-Sham katika mapigano hayo.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

 

Kuna mitazamo miwili kuhusu sababu na chanzo hasa za kuzuka mapigano katika kambi ya Ain Al-Hilweh. Mtazamo wa kwanza ni kwamba, mapigano hayo yametokana na mizozo ya ndani baina ya makundi ya Wapalestina katika kambi hiyo. Lakini mtazamo wa pili, na ambao ndio unaopewa uzito zaidi, ni kwamba mapigano ya Ain Al-Hilweh yametokana na njama. Kambi ya Ain Al-Hilweh, ambayo kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni inahifadhi zaidi ya wakimbizi 63,000 wa Kipalestina, ina mazingira mwafaka ya kuwezesha kukusanyika na kupiga kambi wanachama wa makundi ya Kisalafi kutokana na ukubwa wa kambi yenyewe, idadi kubwa ya watu waliomo ndani yake na kuwemo humo pia njia tata mno na zisizo za kawaida za chini ya ardhi; kiasi kwamba jeshi la Lebanon limekuwa halina uwezo tena wa kuidhibiti kambi hiyo.

Baada ya kuuawa mwanachama wa ngazi ya juu wa harakati ya Fat-h, ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilitangaza katika taarifa kuwa: mauaji yaliyomlenga kamanda wa vikosi vya usalama vya taifa na wasaidizi wake katika kambi za Saida ilikuwa hatua iliyovuka mstari mwekundu. Taarifa hiyo imeeleza kwamba, matukio ya kambi ya Ain Al-Hilweh yanaonyesha kuwa makundi ya kigaidi yanacheza na usalama wa Lebanon na wa kambi hiyo.

Gazeti la Rai Al-Youm limechapisha dokezo kuhusiana na suala hilo linaloeleza kuwa mapigano ya umwagaji damu yaliyozuka kwenye kambi ya Ain Al-Hilweh yanatia shaka; na si baidi utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ukawa umehusika katika fitna hiyo, kwa sababu, -kutokana na kuongezeka nguvu na uwezo wa kuzuia hujuma za kijeshi wa Hizbullah ya Lebanon na kudhoofika kwa jeshi la utawala ghasibu wa Israel kutokana na mivutano na mizozo ya ndani-, kuzuka mivutano na mapigano yoyote ndani ya Lebanon, hususan katika mipaka ya kusini mwa nchi hiyo, kutakuwa ni kwa maslahi ya Tel Aviv.

Mapigano ya namna hii hayamfaidishi yeyote isipokuwa utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Kutokana na kushadidi kwa mapigano, siku ya Ijumaanne, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah alisisitiza juu ya ulazima wa kukomeshwa mapigano katika kambi hiyo. Katibu Mkuu wa Hizbullah alisema: “yaliyotokea Ain Al-Hilweh yanasikitisha na inapasa mapigano hayo yakomeshwe haraka, kwa sababu yana madhara kwa watu wote na yanazilazimisha familia kuhama. Leo, sisi tunawataka watu wote waliopo kambini wasimamishe mapigano. Na kila awezaye kufanya juhudi zozote ili kukomesha mapigano haya, afanye hivyo. Mgogoro huu haupasi kuendelea, kwa sababu matokeo yake yatawaathiri wakazi wa kambi hiyo na watu wote wa kusini mwa Lebanon”.

Kufuatia wito huo wa Sayyid Hassan Nasrullah, Munir Al-Maqdeh mjumbe wa harakati ya Fat-h amesema, kuna makubaliano rasmi ambayo yamefikiwa baina ya pande husika za Lebanon na Palestina kuhusu ulazima wa kutekelezwa usitishaji mapigano katika kambi Ain Al-Hilweh na kisha kufuatiliwa kadhia ya mauaji ya Abu Ashraf Al-Armoushi, mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Fat-h; na kwamba utulivu wa kiwango fulani umerejea katika kambi hiyo ya wakimbizi Wapalestina ndani ya Lebanon…/

Tags