Nov 27, 2023 10:46 UTC
  • Jeshi la Yemen laivurumishia makombora manowari ya US

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) limetangaza habari ya vikosi vya Jeshi la Yemen kuvurumisha makombora mawili ya balestiki na kulenga meli ya kivita ya Marekani ya 'USS Mason' katika Ghuba ya Aden.

Taarifa ya CENTCOM imedai kuwa, makombora hayo ya balestiki ya Jeshi la Yemen yamedondoka mita chache kutoka kwenye manowari hiyo ya Marekani iliyolengwa katika Ghuba ya Aden. 

CENTCOM imesema manowari ya USS Mason imelengwa kwa makombora mapema leo Jumtatu baada ya kujaribu kuisaidia meli ya mizigo ya Israel yenye jina la Central Park iliyoitisha usaidizi. Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, meli hiyo ya Wazayuni ilikuwa imebeba kemikali ya fosforasi,  huku ikiwa na mabahari 22. 

Habari zaidi zinasema kuwa, meli hiyo ya Central Park ilikuwa na bendera ya Liberia, na imekuwa ikiendeshwa na Shirika la Zodiac Maritime lenye makao yake mjini London, ambalo ni sehemu ya Kundi la Mashirika ya Zodiac la bilionea wa Kizayuni, Eyal Ofer.  

Makombora ya balestiki ya Yemen

Haya yanajiri siku chache baada ya vikosi vya majini vya Jeshi la Yemen kufanikiwa kutwaa meli ya Israel katika kina cha Bahari Nyekundu. Watu 52 walioukuwa kwenye meli hiyo yenye jina la 'Galaxy Leader' walikamatwa.

Jeshi la Wanamaji la Yemen limetangaza kwamba litaendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya meli na maslahi ya adui Mzayuni na waungaji mkono wake hadi pale hujuma zake dhidi ya Gaza na jinai zake dhidi ya taifa la Palestina zitakapokomeshwa.

Wiki iliyopita, Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen alisema vikosi vya nchi hiyo vitashambulia na kuteka meli zote zinazomilikiwa au kusimamiwa na kampuni za utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiwa ni hatua kuliunga mkono taifa la Palestina.

Tags