Mar 18, 2024 11:13 UTC
  • HRW: Magharibi inaendelea kuipatia Israel silaha wakati inajadili kupeleka misaada Ghaza

Wakati wabunge katika nchi nyingi za Magharibi wanajadili ni kwa kiwango gani utawala wa Kizayuni wa Israel unaweza ukawa unakwamisha upitishaji misaada ya kuokoa maisha ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza, mauzo ya silaha ambayo yanachangia vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala huo dhidi ya eneo hilo lililowekewa mzingiro yangali yanaendelea kumiminika.

Tangu vilipoanza vita hivyo Oktoba 7, kiwango cha silaha zinazopelekwa Israel kimeongezeka huku sehemu kubwa ya silaha zikitumika kuyadamirisha maeneo ya Ghaza pamoja na kuwaua, kuwatia vilema na kuwafanya wakazi wa eneo hilo wabaki bila makazi.

Akshaya Kumar, Mkurugenzi wa utetezi katika migogoro wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch amesema, "kwa upande mmoja, tuna hitajio hili kubwa la kibinadamu, kwa upande mwingine, tuna usambazaji huu wa kila mara wa silaha kwa nchi ya Israel, inayosababisha hitajio hilo".

Maandamano ya kupinga upelekaji silaha Israel

Kumar amefafanua kwa kusema "wakati hivi karibuni nchi za Magharibi zimekuwa zikifanya juhudi kubwa kuifanya Israel itambue inavyohusika katika kusababisha mateso tunayoyaona huko Ghaza, hatuoni kupunguzwa mtiririko wa silaha kutoka kwa nchi hizo kama Marekani, Ujerumani na nyenginezo".

Nchi wasambazaji wakuu wa silaha kwa Israel zimejikita katika kupeleka misaada huko Ghaza ili kuwafikia Wapalestina wanaoshambuliwa kwa silaha nyingi ambazo nchi hizo zimeupatia utawala huo wa Kizayuni.

Hii ni katika hali ambayo, katika suala la kuipatia nchi nyingine silaha, sheria za kimataifa zimeweka kanuni na mikataba ya kudhibiti nani anampa silaha nani na silaha hizo zinatumika kwa ajili gani.

Chini ya Mkataba wa mwaka 1948 wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari - ambao Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) uliutolea hukumu mnamo Januari kwamba mauaji hayo yanaweza yakawa yanafanyika huko Ghaza - mataifa yanafungwa kisheria kuzuia mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kutokana na kuendelea mwenendo wa kuipatia silaha Israel, wataalamu wa sheria na watetezi wa haki za binadamu wanahoji kama je, nchi za Magharibi haziko hatarini kushtakiwa kwa kosa la kushiriki katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghaza?.../

Tags