Apr 18, 2024 06:21 UTC
  • Mkuu wa UNRWA alaumu vikali hila ya Israel ya kutaka shirika hilo la kusaidia Wapalestina livunjwe

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuwasaidia Wapalestina, UNRWA, Philippe Lazzarini amelaumu vikali kampeni ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kulisambaratisha shirika hilo.

Lazzarini ametoa tamko hilo mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisisitiza kwa kusema: "leo hii, kampeni ya hila ya kuzima operesheni za UNRWA inaendelea, ikiwa na athari kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa".

Lazzarini ameendelea kubainisha kuwa ingawa hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza ingali ni mbaya sana lakini UNRWA inajiona inabanwa kutekeleza majukumu yake kutokana na mamlaka za Israel kuinyima nafasi ya kutoa msaada kaskazini mwa Ghaza licha ya amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ya kuongezwa mtiririko wa misaada katika eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Mkuu huyo wa UNRWA ameeleza kwamba, mamlaka ya shirika lake yanaungwa mkono na mataifa mengi wanachama wa Baraza la Usalama, hata hivyo shirika hilo linakabiliwa na mashinikizo makubwa.

Akifafanua suala hilo, Lazzarini amesema, wanakabiliwa na kampeni ya kufukuzwa kutoka ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kwamba huko Ghaza, serikali ya Israel inataka kukomeshwa shughuli za UNRWA.

Akikosoa vikali uamuzi huo, afisa huyo wa UN amesema, majengo na wafanyakazi wa UNRWA yamekuwa yakilengwa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, na kwamba wafanyakazi 178 wa shirika hilo wameuawa katika mashambulio ya jeshi la utawala huo.

Kwa upande wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Lazzarini amesema, hali ya huko pia ni ya kutia wasiwasi sana kutokana na hatua za kiholela zinazochukuliwa na Israel za kuzuia uwepo na harakati za wafanyakazi wa UNRWA.

Kwa kumalizia hotuba yake, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuwasaidia Wapalestina ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la umoja huo kuhifadhi jukumu muhimu la UNRWA, kwa nchi wanachama kutoa msaada wa kisiasa unaolingana na ufadhili zinaotoa.../

 

Tags