Apr 18, 2024 07:08 UTC
  • Shambulio la makombora la Hizbullah lajeruhi askari 14 wa Israel, sita wako mahututi

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imehusika na shambulio lililolenga kituo cha kijeshi kaskazini mwa 'Israel' na kuwajeruhi wanajeshi wasiopungua 14, na kusema, shambulio hilo limefanywa kulipiza kisasi cha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yaliyoua wanachama wa harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu.

Hizbullah imeeleza katika taarifa kwamba imefanya mashambulizi ya mchanganyiko ya makombora ya kuongozwa kwa mitambo na ndege zisizo na rubani kulenga kituo kipya cha upelelezi wa kijeshi huko Arab al-Aramshe, kijiji kilichoko kaskazini mwa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ambayo imepachikwa jina bandia la Israel karibu na mpaka wa Lebanon.

Jeshi la utawala haramu wa Israel limesema wanajeshi wake 14 walijeruhiwa katika shambulio hilo la jana Jumatano na sita miongoni mwao wako mahututi.

Shambulio hilo la Hizbullah limefanywa siku moja baada ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kusini mwa Lebanon lililoua watu watatu, akiwemo kamanda wa kwenye medani za vita wa Hizbullah aliyetambuliwa na jeshi la Israel kwa jina la Ismail Yusaf Baz.

Siku ya Jumatatu, wanajeshi kadhaa wa utawala haramu wa Israel ambao walivuka mpaka katika ardhi ya Lebanon walijeruhiwa wakati wapiganaji wa Hizbullah waliporipu mada za miripuko, ikiwa ni operesheni ya kwanza ya aina yake kufanywa na harakati hiyo katika miezi sita ya mapigano ya mpakani na jeshi la Kizayuni.

Hizbullah ilitangaza katika taarifa kwamba wapiganaji wake walitega mada za miripuko katika eneo la Tel Ismail kusini mwa Lebanon.../

Tags