Apr 22, 2024 02:33 UTC
  • HAMAS: Msaada mpya wa Marekani kwa Israel ni kwa ajili ya kuendeleza mauaji ya umati

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeilaani Marekani kwa kupasisha msaada mwingine kwa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa msaada huo ni kwa ajili ya kuendeleza mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Shirika la habari la IRNA limenukuu taarifa ya HAMAS iliyotolewa jana Jumapili ikilaani vikali msaada mpya wa Washington kwa utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, hatua ya Bunge la Marekani ya kupasisha msaada huo inazidi kuonesha jinsi dola hilo la kibeberu linavyoshiriki moja kwa moja kwenye mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa kifashisti wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Harakati ya HAMAS imeongeza kuwa, serikali ya Joe Biden huko Marekani inahusika moja kwa moja kisiasa, kisheria na kimaadili katika jinai za kivita za utawala wa Kizayuni.

Wanawake na watoto wadogo wa Palestina, wahanga wakuu wa jinai za Marekani na Israel

 

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania amelaani jinai za Israel na kutaka kukomeshwa mara moja mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza.

Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr ambalo limemnukuu Mohamed Salem Ould Merzoug, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania akisema kuwa nchi yake inasikitishwa sana na hali ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza, na ameitaka Israel ikomeshe jinai zake haraka iwezekanavyo. 

Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri naye ameutaka utawala wa Kizayuni usitishe mara moja mashambulizi yake katika Ukanda wa Ghaza. 

Samih Shokri amesema hayo kwenye taarifa yake rasmi na kuongeza kuwa Misri inaumizwa na hali mbaya waliyo nayo Wapalestina hasa wa Ghaza na jinai zinazofanywa na walowezi wa Kizayuni dhidi ya raia wa kawaida kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina.

Tags