Feb 29, 2020 07:13 UTC
  • Raia wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi wapigwa marufuku kuingia Makka na Madina  kwa sababu ya corona

Saudi Arabia imetangaza kuwa ni marufuku kwa raia wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kuingia katika Haramaini za Makka na Madina, ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi ya kirusi cha corona nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imetangaza kupitia taarifa iliyotoa usiku wa kuamkia leo kuwa, sheria ya kuweka marufuku kwa raia wa nchi hizo za Kiarabu kuingia Makka na Madina ni ya muda na haitawahusu watu ambao wamekuwapo nchini humo kwa muda wa wiki mbili.

Saudi Arabia imetangaza pia kwamba, utoaji viza ya matembezi kwa raia wa nchi ambazo zimekumbwa na kirusi cha corona umesimamishwa.

Saudia imesitisha Ibada ya Umra kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya kirusi cha corona

Minong'ono ya kuzuka mripuko wa kirusi cha corona katika eneo la Asia Magharibi ilianza kusikika kwa mara ya kwanza nchini Saudia, ambapo tarehe 6 ya mwezi uliopita wa Februari vyombo vya habari vya nchi hiyo vilitangaza kuwa raia wawili wa India wanaoishi nchini humo wamekumbwa na kirusi hicho, lakini muda mfupi tu baadaye viongozi wa Riyadh walikadhibisha habari hiyo.

Mripuko wa kirusi cha corona ulianzia katika mji wa Wuhan ulioko katika mkoa wa Hubei nchini China Desemba mwaka uliopita wa 2019.

Mbali na mikoa 30 ya China, hivi sasa kirusi hicho kimeshaenea kwenye zaidi ya nchi nyingine 55 duniani.../

Tags