Dec 24, 2022 06:26 UTC

Mafuriko makubwa yaliukumba mji mtakatifu wa Makkah nchini Saudi Arabia siku ya Ijumaa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku, kuharibu magari na mali katika mji huo.

Picha za video za mafuriko hayo zimeonyesha magari yakisombwa na mafuriko ya maji, huku barabara kuu kadhaa zikifungwa.

Mji wa Makka ulishuhudia mvua kubwa Alhamisi usiku hadi Ijumaa asubuhi. Kituo cha Kitaifa cha Utabiri wa Hali ya Hewa kilitoa onyo la hali ya hewa katika jimbo la Makka siku ya Ijumaa huku mvua ikiendelea kunyesha kwa viwango vya wastani hadi vya juu katika maeneo ya Rania, Taif, Adham na Maysan.

Picha za video kutoka Msikiti Mkuu wa Makka zilionyesha mvua ikinyesha huku waumini wakiwa wanaendelea na ibada ya Hija ndogo ya Umrah.

Uwanja wa ndege wa Mfalme  Abdulaziz mjini Jeddah uliwaomba wasafiri wapige simu ili kuthibitisha hali ya safari zao za ndege kabla ya kuelekea uwanja wa ndege, kwani baadhi ya safari za ndege zilitarajiwa kusitishwa kutokana na hali mbaya ya hewa.

Kituo cha utabiri wa hali ya hewa pia kilionya kuhusu mafuriko na ngurumo zinazoambatana na mvua kubwa katika mkoa wa Jeddah ulio kaskazini mwa Makka.

Mnamo Novemba, watu wawili walikufa katika mafuriko ambayo yalikumba mji wa pwani wa Jeddah kutokana na mvua kubwa ambazo hazijawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu mjini humo.

Tags