Jan 12, 2024 08:05 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran azungumza na mawaziri wenzake wa Saudia na Norway kuhusu Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na Norway kuhusiana na kupanua uhusiano wa pande mbili na matukio yanayojiri katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa IRNA, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia Hossein Amir-Abdollahian na Faisal Bin Farhan wamejadili baadhi ya masuala yenye maslahi kwa nchi mbili katika uga wa uhusiano wa pande mbili na matukio ya hivi karibuni ya Palestina.

Katika mazungumzo hayo waliyofanya usiku wa kuamkia leo, Amir-Abdollahian, amesema uhusiano wa kisiasa kati ya nchi mbili uko kwenye mkondo sahihi na akaashiria hatua ya Saudi Arabia ya kuitisha kikao cha wakuu wa nchi za Kiislamu na Kiarabu kwa lengo la kusimamisha vita vya Gaza na kutuma misaada ya kibinadamu katika eneo hilo na akasisitiza kwa kusema: "tunaunga mkono hatua ya Afrika Kusini ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia kuendelea kwa jinai za Wazayuni za mauaji ya wananchi wa Palestina na akabainisha kuwa: kwa muda wa karibu siku 100, Marekani imekuwa ikizungumzia kutopanuliwa vita hivyo, lakini kivitendo haionyeshi kuwa inalipa uzito wowote suala la kusimamisha vita na mauaji ya kimbari huko Gaza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan amesema, uhusiano wa Riyadh na Tehran unaendelea kupanuka na akaashiria mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kusema: "tuendelee kadiri iwezekanavyo kushinikiza ili vita dhidi ya Gaza vikomeshwe".

Waziri Abdollahian na mwenzake wa Norway Spenbart Aid

Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo na mwenzake wa Norway, Spenbart Aid, ambapo mbali na kuipongeza serikali na watu wa Norway kwa kuanza mwaka mpya wa Miladia, amesema kuendelea kufanywa mashauriano kati ya Tehran na Oslo kutapelekea kupanuka uhusiano katika nyanja zenye maslahi kwa pande mbali; na sambamba na kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza amepongeza hatua ya Afrika Kusini ya kuwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Kizayuni na akasema: mauaji ya kimbari ya Gaza na Ukingo wa Magharibi pamoja na mzingiro dhidi ya watu vikomeshwe haraka.../

 

Tags