Feb 22, 2023 02:32 UTC
  • Taarifa rasmi ya Baraza la Usalama ya kulaani vitongoji vya walowezi

Jumatatu ya tarehe 20 Februari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha rasimu ya azimio linalolaani uamuzi wa serikali ya Israel yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa ya baraza hilo iliyosomwa juzi Jumatatu na Vanessa Frazier, Mwakilishi wa Kudumu wa Malta katika Umoja wa Mataifa ilisema: Baraza la Usalama linakariri kuwa, kuendeleza ujenzi wa vitongoji kunakofanywa na Israel kunauweka hatarini uwezekano wa kufikia suluhu baina ya Israel na Palestina kwa misingi ya mipaka ya 1967. 

Amesema Baraza la Usalama limetiwa wasiwasi na tangazo la Februari 12 la Israel, kwamba utawala huo utafanya upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Baraza la Usalama limesema tangazo hilo la serikali ya Netanyahu la kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linaweka vizingiti zaidi katika barabara ya kusaka amani ya kudumu na endelevu.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua hii ni pigo jipya kwa njama za serikali mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel yenye misimamo mikali inayoongozwa na Benjamin Netanyahu, za kupora ardhi zaidi za Palestina.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni

 

Hatua hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imejiri miaka sita baada ya azimio la mwisho la baraza hilo ambapo Marekani wakati huo pia ilijizuia kupiga kura.

Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2016 ambapo serikali ya Barack Obama Rais wa wakati huo wa Marekani ilijizuia kulipigia kura azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama lililokuwa likiutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina. Hatua hiyo ya Marekani sambamba na nchi za Ulaya wanachama wa Baraza la Usalama ya kulipigia kura ya ndio azimio hilo iliikasirisha mno Israel.

Misimamo ya mataifa hayo yanayohesabiwa kuwa waitifaki wakongwe wa Israel inaonyesha kuwa, kuendelea siasa zisizo za kibinadamu na zilizo kinyume cha sheria za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hazihalalishiki na si za kimantiki hata kwa waitifaki wa Magharibi wa utawala huo ghasibu.

Ni kutokana na ukweli huuo ndio maana mataifa haya hayana budi isipokuwa kuwa pamoja na jamii ya kimataifa katika misimamo yake ya kupinga hatua za utawala vamizi wa Israel.

Ujumbe wa Israel ukitolewa nje ya mkutano baada ya kufahamika kwamba, umeingia katika mkutano huo kinyume cha sheria

 

Azimio hilo kwa mara nyingine tena limethibitisha kwamba, kitendo cha Israel cha kujenga vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1967, ikiwemo Mashariki ya mwa al-Quds, si halali na ni kinyume cha kisheria, na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

 Riyadh Mansur, mwakilishi wa Palestinja amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuipa umuhimu kadhia ya Palestina na kutoipuuza.

Nukta ya kuzingatia zaidi ni kuwa, hata baina ya Mayahudi pia kumekuweko na upinzani unaoongezeka dhidi ya hatua zinazochukuliwa na utawala ghasibu wa Israel huko Palestina.

Inaonekana kuwa, licha ya Marekani kujitutumia na kuupigia kifua utawala wa Kizayuni kila leo, lakini kivitendo mambo yanazidi kuuendea kombo utawala huo hasa kutokana na kutengwa kimataifa. Mashinikizo dhidi ya utawala huo ghasibu yanaongezeka kila uchao huku walimwengu wakiutenga zaidi na kuulaani kila kona.  Mfano wa karibu kabisa ni kutimuliwa kidhalili ujumbe wa Israel katika mkutano wa Umoja wa Afrika ulioingia kilaghai katika kikao cha Umoja wa Afrika.

Tags