Faili la Trump-Russia na mpasuko wa kisiasa ndani ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i29316-faili_la_trump_russia_na_mpasuko_wa_kisiasa_ndani_ya_marekani
Rais Donald Trump wa Marekani amekosoa kwa njia isiyo ya wazi hatua ya kuteuliwa Mwanasheria Maalumu wa kushughulikia faili la tuhuma za kuingilia Russia uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka jana nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2017 23:33 UTC
  • Faili la Trump-Russia na mpasuko wa kisiasa ndani ya Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani amekosoa kwa njia isiyo ya wazi hatua ya kuteuliwa Mwanasheria Maalumu wa kushughulikia faili la tuhuma za kuingilia Russia uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka jana nchini Marekani.

Trump amesema, uamuzi huo unaipasua nchi vipande viwili. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya White House, kwa mara nyengine tena Donald Trump amekana kuwepo ushirikiano wowote wa siri baina yake na wajumbe wa timu yake ya kampeni na serikali ya Russia wakati wa kinyangányiro cha uchaguzi wa rais wa Marekani.

Rais Donald Trump

Wakati huohuo vyombo vya habari vimeripoti kuwa ndani ya muda wa miezi sita, wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika mwaka jana, wajumbe wa timu ya kampeni ya uchaguzi ya Donald Trump waliwasiliana mara zisizopungua 18 na Russia kwa njia ya simu na baruapepe. Kuna dhana na tetesi mbali mbali kwamba katika mazungumzo na mawasiliano hayo timu ya Trump ilibadilishana taarifa za siri na Warusi na kuwekeana ahadi za mambo kadhaa. Hivi sasa kwa uchache imebainika kuwa Michael Flynn, aliyekuwa wakati huo mjumbe wa timu ya kampeni ya Trump na mshauri wake wa kwanza wa usalama wa taifa, aliwasiliana na balozi wa Russia mjini Washington na kumwahidi kuondolewa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo na Marekani, tena basi katika siku ileile ambapo rais wa wakati huo Barack Obama alikuwa amesaini vikwazo vipya dhidi ya Russia kwa kisingizio cha Moscow kuingilia uchaguzi wa Marekani. 

Michael Flynn

Hivi sasa Rais wa Marekani anakabiliwa na tuhuma za kuwa na mashirikiano ya siri na Russia, ambayo inatizamwa kama nchi adui na akthari ya wenye vipawa vya kisiasa wa Marekani na tapo kubwa la fikra za waliwengi nchini humo. Uamuzi wa kuteua mwanasheria maalumu uliochukuliwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani ambao umefanyika pasina kuishauri Ikulu ya White House wala Trump mwenyewe kama rais, umemuudhi na kumkasirisha kiongozi huyo. Katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema serikali yake inatendewa dhulma kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani; na ndiyo maana ametahadharisha juu kupasuka nchi vipande viwili na kudai kuwa wapinzani wake wana nia ya kuiangusha serikali yake.

Paul Ryan

Kwa sasa haionyeshi kuwa maonyo na malalamiko ya mara kwa mara ya Trump yameweza kuwa na tija inayokusudiwa na White House. Msimamo wa Paul Ryan, Spika wa Baraza la Wawakilishi na kiongozi wa juu kabisa wa chama tawala cha Republican katika Kongresi ya Marekani, wa kuunga mkono kufanyika uchunguzi huru kuhusu "Faili la Trump-Russia" umeibua wasiwasi wa kujitenga bunge la Marekani na Ikulu ya White House katika moja ya mafaili nyeti na hasasi zaidi ya kisiasa kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya karibuni nchini humo. Hapana shaka kuwa wabunge wengi wa chama cha Republican hususan viongozi wa chama hicho wangali wako nyuma ya Trump na wanajaribu kuhakikisha joto la sakata linalomkabili kiongozi huyo halitokoti zaidi. Lakini pamoja na hayo si hasha uchunguzi unaotazamiwa kufanywa na Mwanasheria Maalumu Robert Mueller, ambaye ni mkuu wa zamani wa Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI ukafichua taarifa nyengine mpya na kuitia doa zaidi serikali ya nchi hiyo na hasa Rais Trump mwenyewe.

Robert Mueller

Alla kulli hal, lililo wazi ni kuwa hivi sasa jamii ya Marekani imegawika mapande mawili na kuwa na mpasuko mkubwa zaidi ya ilivyokuwa wakati wa uchaguzi wa rais. Wakati ule jamii ya Wamarekani ilikuwa imezungukwa na wagombea wawili, ambao kila mmoja alikuwa na muelekeo na mtazamo tofauti na wa mwenzake kwa ajili ya kuongoza nchi hiyo. Lakini hivi sasa jamii hiyo inakabiliana na kadhia mpya, ambapo katika upande wake mmoja kuna rais na serikali yake na katika upande mwengine kuna rundo la taarifa za tuhuma za uhalifu, mawasiliano ya siri na ulaji njama kwa kushirikiana na Russia.

Inatabiriwa kuwa hadi pale ukweli wa mambo kuhusiana na faili hilo lenye utata mkubwa utakapodhihirika, mpasuko wa kisiasa ndani ya Marekani utazidi kuwa mpana na mgawanyiko uliopo wa hali ya matapo mawili utakuwa mkubwa zaidi.../