Takwimu Jumapili
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i2953-takwimu_jumapili
Leo ni Jumapili tarehe tatu Jamaduth-Thani 1437 Hijria, inayosadifiana na tarehe 13 Machi, 2016 Miladia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2016 01:52 UTC
  • Takwimu Jumapili

Leo ni Jumapili tarehe tatu Jamaduth-Thani 1437 Hijria, inayosadifiana na tarehe 13 Machi, 2016 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 1426 iliyopita, sawa na tarehe tatu Jamaduth-Thani mwaka wa 11 Hijiria, alifariki dunia Bibi Fatwimat Zahraa (as), binti wa Mtume Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali Bin Abi Twalib (as), baada ya muda mfupi wa maisha yake. Bibi Fatwimat Zahraa alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa na Mwenyezi Mungu Mtume wa Allah. Mama yake Bibi Fatwimat Zahraa ni Bibi Khadija Binti Khuwailid (as) mwanamke mtakatifu na aliyekuwa akipendwa sana na Nabii wa Allah (saw). Chini ya malezi ya baba yake, Bibi Fatwima alifikia daraja la juu katika maarifa, elimu na uchaji-Mungu. Katika maisha yake, Bibi huyo mtukufu alifahamika sana kwa ukarimu, kujitolea, subira, kutosheka, uchaji-Mungu na kuwasaidia masikini na watu wasiojiweza. Bibi Fatwima Zahraa aliishi miezi michache tangu alipofariki dunia baba yake Mtume Muhammad (saw). Aidha Bibi huyo, alijishughulisha na kuwalea wanawe yaani Imam Hassan na Imam Hussein (as) ambao wametajwa na Bwana Mtume kuwa ni Mabwana wa Vijana wa Peponi. Wasomi wengi wamemzungumzia Bibi Fatwima (as) na kumtaja kuwa kigezo bora cha jamii na shaksia ya mwanamke mkamilifu wa Kiislamu. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa msiba huu mchungu wa kumpoteza mtukufu huyo.

Siku kama ya leo miaka 283 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mwanakemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia. Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea kwa gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 63 Aalim na mtafiti wa Kiislamu Mir Sayyid Hassan Mudarris Isfahani. Mir Sayyid alizaliwa mwaka 1210 Hijiria mjini Isfahan na baada ya kusoma masomo ya awali ya kidini kama vile fiq’hi na usuul fiq’hi, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu kiitwacho “Jawaamiul-Kalaam” na “Sherehe ya Kitabu cha Shifa cha Abu Ali Sina.”

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran. Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa. Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika bunge la Taifa.

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah, walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyohiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmuun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel, yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya Uingereza katika eneo hilo.