Imamu Khomeini, mpiganaji mwanamapinduzi na mwanamuqawama
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i29996-imamu_khomeini_mpiganaji_mwanamapinduzi_na_mwanamuqawama
Tarehe 14 Khordad sawa na tarehe nne Juni inasadifiana na kumbukumbu ya mwaka wa 28 wa kufariki dunia Imamu Khomein (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2017 21:59 UTC
  • Imamu Khomeini, mpiganaji mwanamapinduzi na mwanamuqawama

Tarehe 14 Khordad sawa na tarehe nne Juni inasadifiana na kumbukumbu ya mwaka wa 28 wa kufariki dunia Imamu Khomein (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku hiyo, taifa la Iran na wapenzi wote pamoja na wafuasi wa njia na fikra za Imam Khomeini huwa wanamkumbuka mwanachuoni huyo mkubwa. Moja ya vitu muhimu vilivyoshuhudiwa katika maisha ya Imam Khomeini (MA) ilikuwa ni kueneza fikra ya kimapinduzi kwa lengo la kuyaamsha mataifa yanayodhulumiwa katika kukabiliana na tawala za kidhalimu na kusimama imara kupambana na dhulma. Imam Khomeini kwa kuegemea misingi miwili muhimu, ambayo wa kwanza ni kutosalimu amri na kutoogopa mmbele ya vitisho huku wa pili ukiwa ni mwamko wa kupambana na ukoloni, masuala ambayo yameleta mwamko mkubwa nchini Iran na kwa mataifa yanayopigania ukombozi duniani.

Harakati za mapinduzi nchini Iran miongo minne iliyopita

Kwa harakati hizo kubwa, Imam Khomeini aliweza kufichua uhakika mbalimbali katika kipindi cha mapambano yake ambapo mwenyewe aliamini na kutegemea roho ya kimapinduzi na aliweza kufikia malengo makubwa na ushindi. Ni kwa ajili hiyo na ni kwa kuzingatia kuwa Imam Khomeini alikuwa na welewa wa mambo ulioambatana na kutotetereka, ndipo akaweza kusimama imara kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Shah uliokuwa umejizatiti kwa kila namna. Sifa hiyo ya Imam Khomeini MS kwa hakika, hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya maadui wote kupiga kambi upande mmoja kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu na kusimama dhidi ya shakhsia ya Imam Khomeini (MA.) Imam aliweza kuongoza Mapinduzi kwa kusimama imara dhidi ya utawala muovu wa dikteta Shah nchini Iran, huku akipuuza vitisho mbalimbali ikiwemo kubaidishwa na ukandamizaji mwingine mkubwa aliofanyiwa na watawala wa wakati huo. Imani ya kimapinduzi aliyokuwa nayo Imam Khomeini MA iliandaa mazingira ya mabadiliko makubwa nchini Iran kiasi cha kulifanya taifa hili hii leo kuwa kiigizo chema duniani.

Imam Khomeini MA katika moja ya hotuba zake muhimu

Kiigizo ambacho si tu kimeiletea Iran mabadiliko na maendeleo makubwa, bali pia kimeonesha njia ya kimapinduzi na harakati ya mwamko wa Kiislamu duniani. Katika vipindi vyote vya mapambano, ambapo Imam Khomeini (MA) alishikamana vilivyo na moyo wa mapambano, sambamba na kukabiliwa na mazingira magumu na ukandamizaji mkubwa wa kisiasa wa utawala wa Shah lakini aliendelea kufichua njama chafu za uistikbari wa Marekani na malengo machafu ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati. Sababu ya uadui wa Marekani kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ni msimamo imara kwa taifa la Iran dhidi ya uingiliaji wa Washington na kupenda kwake kujitanua duniani.

Imam Khomeini (MA)

Aidha kutokana na madola ya kibeberu na yenye kupenda kujitanua kuwa na wasi wasi mkubwa, yaliamua tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kuendesha njama na harakati kubwa za kuikwamisha na kuimaliza harakati hiyo adhimu. Pamoja na njama zote hizo, lakini maadui hao wameshindwa kukwamisha safari hiyo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita Marekani imeweka vikwazo na kufanya njama za kila aina kwa visingizio tofauti dhidi ya Iran ya Kiislamu. Washington pia inaendesha njama za kuzusha mizozo ndani na nje ya Iran ili kuzuia maendeleo ya taifa hili na kufanikishwa malengo matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo taifa la Iran na kwa kushikamana na matukufu ya kimapinduzi na malengo matakatifu ya Imam Khomeini (MA) wameweza kuzishinda njama zote chafu za maadui hususan Marekani.