Siku ngumu za vita vya Saudia dhidi ya taifa la Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i32484-siku_ngumu_za_vita_vya_saudia_dhidi_ya_taifa_la_yemen
Katika mwezi wa 29 wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen na licha ya hali mbaya sana inayoshuhudiwa nchini humo, jeshi la Yemen likishirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah, limetoa kipigo kikali kwa utawala wa Aal-Saud na kuzifanya siku za vita hivyo kuwa ngumu kwa Riyadh na washirika wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2017 23:56 UTC
  • Siku ngumu za vita vya Saudia dhidi ya taifa la Yemen

Katika mwezi wa 29 wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen na licha ya hali mbaya sana inayoshuhudiwa nchini humo, jeshi la Yemen likishirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah, limetoa kipigo kikali kwa utawala wa Aal-Saud na kuzifanya siku za vita hivyo kuwa ngumu kwa Riyadh na washirika wake.

Tarehe 28 ya mwezi huu, jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah lilishambulia na kudhibiti kambi ya jeshi ya al-Jabiri na maeneo ya al-Faridha, Malhamat na al-Ghawiyah yaliyopo mji wa Jizan, kusini mwa Saudia. Vilevile askari kadhaa wa utawala wa Aal-Saud wameangamizwa na wengine kujeruhiwa na zama zao zimeharibiwa. Alkhamisi iliyopita pia kikosi cha jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah kilivurumisha makombora kadhaa ya masafa ya kati ya Burkan-1 na kulenga kambi ya Jeshi la Anga ya Mfalme Fahd bin Abdulaziz Al Saud iliyopo mji wa Taif. Kambi hiyo imeteketezwa kwa moto mkubwa ulioshuhudiwa kambini hapo.

Moja ya makombora ya jeshi la Yemen lililofyatuliwa kushambulia kambi ya jeshi la anga ya Saudia

Hakuna shaka kwamba hali ya mambo nchini Yemen imezidi kuwa mbaya. Watu wasiopungua elfu 12 wameuawa moja kwa moja na vita hivyo visivyo na mlingano, na makumi bali mamia ya maelfu ya wengine wakiwa wanakaribia kupoteza maisha yao kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita hivyo. Kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu na mgogoro mkubwa wa ukosefu wa chakula ambayo ni matokeo ya vita hivyo, ni kielelezo cha hali mbaya ya nchini Yemen.

Katika uwanja huo Bismarck Swangin, mtaalamu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen amenukuliwa akisema: "Vita nchini Yemen ni vita dhidi ya watoto wadogo ambao kutokana na lishe duni wanasubiri kifo na mauti, na mbaya zaidi ni kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo.

Kifo kinawanyemelea watoto wa Yemen kutokana na jinai za Saudia

Watoto wa Yemen si tu kwamba ni wahanga wa mashambulizi ya moja kwa moja ya mabomu ya Saudia, bali pia ni akthari yao wanakaribia kufariki dunia kutokana na athari mbaya za vita hivyo". Bismarck Swangin anaendelea kusema kuwa: "Inatosha tu kutazama hospitali na vituo vya afya vya nchi hiyo masikini ya Waislamu wa Yemen ili upate kuelewa hisia za mama anayemuangalia mtoto wake alili na mgonjwa aliyelala chini bila ya kuwa na matumaini ya aina yoyote. Akina mama hao hawana matumaini tena, wamemuachia hatma yao Mwenyezi Mungu pekee na hiyo ndio hali yao", mwisho wa kunukuu.

Kwa sasa jeshi la Yemen haliwezi kuondoa hali hiyo kwa kuwa taifa hilo hivi sasa limewekewa mzingiro wa kila upande wa Saudia na washirika wake, ingawa katika upande wa kijeshi limeweza kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Aal-Saud.

Watoto wanouawa moja kwa moja na Saudi Arabia huko Yemen

Kudhibitiwa kambi za jeshi za mji wa Jizan, kuangamizwa makumi ya vibaraka wa Saudia na kadhalika kuishambulia kwa makombora kambi ya Jeshi la Anga ya Mfalme Fahd bin Abdulaziz Al Saud ya mji wa Taif katika kipindi cha siku mbili tu zilizopita, ni sehemu ya mapigo makali yaliyoikumba Riyadh katika kipindi cha miezi 28. Inaonekana kuwa, jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah bado ni nguvu kubwa na imara licha ya kupita miezi 28 ya vita. Hali hiyo inaweza kwa mara nyingine kuifanya Marekani izidishe kiwango cha uungaji mkono na misaada yake kwa Saudia.

Kombora la Burkan 1 ambalo limeitia kiwewe Saudia

Katika uwanja huo, Sayyid Hussein Musawiyan mtafiti wa Chuo Kikuu cha Princeton nchini Marekani ambaye pia mtaalamu wa masuala ya kimataifa amesema kuwa, Marekani ni mshirika wa jinai na ukatili unaofanywa na Saudia dhidi ya Yemen. ameongeza kuwa: "Lau kama si uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa Saudia, Riyadh isingeweza kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya taifa hilo la Kiarabu hadi sasa."

Natija tunayoipata ni hii kwamba, vita nchini Yemen vimefikia katika hali nzito kwa pande zote hususan Saudi Arabia, kwa kuwa hivi sasa Riyadh inaandamwa na mashinikizo ya fikra za waliwengu kutokana na hali mbaya inayoshuhudiwa nchini Yemen, na katika upande mwingine imepata kipigo na hasara kubwa kutokana na kuimarika zaidi uwezo wa kijeshi na hata makombora ya jeshi la Yemen na harakati ya wananchi ya Answarullah.