Hija kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i32498-hija_kwa_mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu_wa_mapinduzi_ya_kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumapili ya jana tarehe 30 Julai alikutana hapa mjini Tehran na maafisa na wasimamiaji wa amaji ya Hija ya mwaka huu na kusema kuwa, ibada ya Hija ni fursa ya kutangaza misimamo na maudhui zinazokubaliwa na Umma wa Kiislamu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jul 31, 2017 02:16 UTC
  • Hija kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumapili ya jana tarehe 30 Julai alikutana hapa mjini Tehran na maafisa na wasimamiaji wa amaji ya Hija ya mwaka huu na kusema kuwa, ibada ya Hija ni fursa ya kutangaza misimamo na maudhui zinazokubaliwa na Umma wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria kiburi cha Wazayuni ambao wamejipa haki ya kuwawekea vizingiti wamiliki wa Msikiti wa al-Aqswa na kuwazuia na kusema bayana kwamba: Kwa namna yoyote ile haipaswi kughafilika na kadhia ya Palestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Ni mahala gani bora kuliko Beitullah al-Haraam (Nyumba ya Mwenyezi Mungu), Makka, Madina, Arafa, Mash'ar al-Haraam  na Mina  kwa ajili ya kuonyesha itikadi na kubainisha misimamo ya mataifa ya Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina na Masjid al-Aqswa?"

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Matamshi ya Kiongozi Muadhamu kuhusiana na Hija hususan upande wa kukumbusha kadhia ya Palestina na Quds Tukufu, ni jambo linaloonyesha nafasi muhimu na athirifu iliyonayo ibada ya Hija kwa mustakabali wa Ulimwengu wa Kiislamu katika pande mbalimbali. Hii leo eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na changamoto kubwa kama harakati za makundi ya kigaidi na kitakfiri ambapo mataifa ya Kiislamu yanapaswa kutangaza misimamo yao katika Hija.

Muhammad Reza Khoshroo, mtaalamu na mtafiti katika masuala ya "Hija na vyombo vya habari " alisema katika mahojiano aliyofanyiwa kwamba: Hija ni mahala pa kudhihirisha umoja na kuonyesha mfungamano wa nyoyo za Waislamu pamoja mshikamano dhidi ya maadui. 

Hapana shaka kuwa, Hija ni faradhi yenye uwezo wa kuonyesha adhama ya Umma wa Kiislamu na kuzipa changamoto tawala fasidi ambazo zinaona kuwa, kubakia kwao kunafungamana na kutekeleza matakwa ya mabeberu na kuwa washirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwasalimia viongozi na watendaji wa masuala ya Hija

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesea kuwa, kuna udharura kwa mataifa ya Kiislamu kulipa umuhimu suala la umoja ambalo ni muhimu sana na akaongezea kuwa, katika hali ambayo, mamilioni ya dola yanatumika kwa ajili ya kuzusha hitilafu, mifarakano na uadui miongoni mwa Waislamu, wafuasi wa dini hii tukufu wanapaswa kuwa macho ili wasije wakasaidia kusukuma mbele gurudumu la malengo ya maadui hao.

Nchi za Kiislamu zinapaswa kutambua vyema na kwa njia sahihi chimbuko la migogoro na kudiriki ukweli wa mambo. Lengo la Uistikbari wa dunia ni kuzusha machafuko na ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati na hivyo kuwafanya watu waghafilike na hivyo kuisahau kadhia ya Palestina.

Utawala wa Kizayuni wa Israel uliibuka katika anga iliyokuwa na vumbi huko Syria, Yemen, na Iraq na kutumia fursa hiyo kutenda jinai kubwa dhidi ya wananchi wa Palestina na hivyo kushadidisha siasa zake za kupenda kujitanua na jinai dhidi ya wananchi hao madhulumu. 

Baadhi ya maafisa na wasimamiaji wa amaji ya Hija 

Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya kiislamu amekumbusha kuwa, Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ndio wenye ushari na ukhabithi zaidi kuliko harakati zozote za kigaidi.

Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na umuhimu wa kongamano kubwa la Hija katika kufichua na kusambaratisha njama za ubeberu, Uistikbari na Uzayuni katika Mashariki ya Kati ni jambo linaloonyesha upeo mkubwa wa kifikra na kuwa na mtazamo mpana juu ya umuhimu wa kiistratejia wa Hija katika pande mbalimbali.

Hapana shaka kuwa, kuna haja ya kutumia vyema fursa hii yenye thamani kwa ajili ya kuinua na kupanua nguvu za Ulimwengu wa Kiislamu. Hii ni kutokana na kuwa, Hija ni ya Waislamu wote ambao wana uwezo mkubwa zaidi wa kijamii na kisiasa katika nyuga zote na ni mahala pa kuonyesha itikadi na misimamo ya Umma wa Kiislamu na  wakati huo huo ni dhihirisho la umoja wa Kiislamu.