Udiplomasia wa kilaghai wa Saudi Arabia kuhusu Iraq
Msemaji wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq cha Hashdu Sha'abi, Ahmad al Asadi amesema kuwa serikali ya Saudia imeigeukia Iraq ili kujiondoa katika mzingiro wa kisaikolojia katika eneo hili la Mashariki ya Kati.
Al Asadi ameongeza kuwa viongozi wa Saudi Arabia wanafanya jitihada za kujikurubisha kwa Iraq ili kukabiliana na matatizo makubwa yanayowakabili ikiwa ni pamoja na kushindwa nchi hiyo huko Yemen. Kushindwa na kufeli huko kwa serikali ya Riyadh huko Yemen kumekuwa na taathira katika uga wa kimataifa na kieneo. Vita vikubwa vya Saudia na hatua zake za kuingilai kati na kuzusha fitna katika eneo la Mashariki ya Kati kupitia njia ya kuwaunga mkono magaidi wa kitakfiri kumeifanya nchi hiyo itengwe zaidi kimataifa na kudhoofika nafasi yake katika eneo hili kiasi kwamba, hivi sasa Saudia haina tena ushawishi mkubwa katika taasisi zilizo chini ya udhibiti wake yaani Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na hata katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab Legue). Aidha hitilafu na mivutano mikubwa inayoshuhudiwa sasa ndani ya Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi zinathibitisha ukweli huu. Hali hii imeilazimisha Saudia kuboresha kwa kiasi fulani uhusiano wake na baadhi ya nchi hza Kiarabu. Ni wazi kuwa uhusiano baridi wa Saudi na Iraq umeboreka katika miezi ya hivi karibuni baada ya safari ya Adel al Jubairi Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia huko Baghdad. Hata hivyo ushahidi uliopo, uingiliaji mpya na njama zinazofanywa na Saudia, yote yanadhihirisha namna Iraq inavyoendelea kukabiliwa na udiplomasia wa kilaghai wa utawala wa Aal Saud.
Awali Saudia haikuupa obalozi wake nchini Iraq umuhimu wa kistratijia na hatimaye Thamer al Sabhan ambaye alikuwa Balozi wa Saudia mjini Baghdad alifukuzwa nchini humo kwa sababu ya kuingilia masuala ya ndani ya Iraq. Balozi huyo wa zamani wa Saudia mjini Baghdad alikuwa akivishambulia na kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq. Wakati huo duru mbalimbali za Iraq zilitangaza habari ya kuwepo nyaraka zilizofichua mahusiano yaliyokuwepo kati ya Thamer al Sabhan na kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq.
Saudi Arabia ambayo inaona kuwa siasa zake katika eneo la Mashariki ya Kati hususan huko Iraq zimegonga mwamba, hivi sasa imeamua kutumia mbinu mbalimbali ili kuficha kushindwa kwake na wakati huo huo isogeze mbele siasa zake za ghilba na hila huko Iraq baada ya kuondoka kundi la Daesh.
Katika mazingira kama hayo, Saudia inataka kujipenyeza katika maeneo mbalimbali ya Iraq lengo likiwa ni kuzusha fitna na mgawanyiko miongoni mwa matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iraq. Mawasiliano yenye kutia shaka kati ya viongozi wa Saudia na wa eneo la Kurdistan la Iraq na pia hatua za Riyadh za kutaka kufungua balozi zake ndogo katika maeneo mbalimbali ikiwemo huko Najaf na kufanyika mashauriano kati ya Saudia na viongozi wa baadhi ya makundi ya Kiiraqi akiwemo Muqtada Sadr, yote hayo yanadhihirisha kusudio kuu la Saudi Arabia la kutaka kufanya njama na kuzusha mgawanyiko zaidi huko Iraq.
Katika upande mwingine, Saudi inatambua vyema nukta hii kwamba, zama za magaidi wa kitakfiri likiwemo kundi la kigaidi la Daesh ambalo linaungwa mkono kwa hali na mali na utawala wa Aal Saud huko Iraq zimekwisha. Kwa msingi huo, viongozi wa Saudia wanafanya kila wawezalo ili kuandaa uwanja wa kukisambaratisha kikosi cha Hashdu Sha'abi katika duru mpya ya kutaka kuingilia masuala ya ndani ya Iraq.
Matukio yanayojiri huko Iraq yanaleta udharura zaidi kwa makundi na shakhsia wa Iraq kuchukua tahadhari mkabala na udiplomasia wa kilaghai ulioanzishwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo.