Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia nchini Ethiopia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amewasili Addis Ababa kwa shabaha ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Ethiopia.
Akiwa Addis Ababa, Sergei Lavrov atakutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, Waziri Mkuu wa Ethiopia na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo kwa shabaha ya kuimarisha uhusianio na ushirikiano wa pande hizo. Safari hiyo ya Sergei Lavrov nchini Ethiopia inafanyika sambamba na ile mwenzake wa Marekani, Rex Tillerson nchini humo na katika nchi nyingine kadhaa za Afrika.
Kwa muda mrefu sasa Russia imekuwa ikifanya mikakati ya kupanua zaidi uhusiano wake na nchi za Afrika. Viongozi wa ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin wanakusudia kuimarisha zaidi uhusiano na nchi mbalimbali za bara hilo katika nyanja za uchumi, siasa na masuala ya kijeshi. Katika upande wa masuala ya uchumi, makampuni ya Russia hususan katika sekta ya mafuta na gesi yana mipango ya kutaka kufunga mikataba ya muda mrefu na kuwekeza katika masoko ya Afrika. Suala hili la kustawisha uchumi na kuzidisha ushirikiano na nchi nyingi za Afrika ikiwemo Ethiopia lina umuhimu mkubwa kwa Russia. Nchi nyingi za Afrika zinafanya jitihada za kuboresha uchumi wao, kupambana na umaskini na kujenga miundombinu imara, suala ambalo linaweza kutayarisha mazingira mazuri zaidi ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao na Russia.
Katika upande wa masuala ya kisiasa pia Russia iko mbioni kuboresha nafasi yake katika mfumo wa kimataifa na kuzidisha ushawishi wake barani Afrika mkabala wa wapinzani wake wakuu kama Marekani na nchi za Ulaya. Kwa sasa Afrika imekuwa uwanja mkubwa wa ushindani wa madola makubwa duniani kutokana na utajiri wake wa maliasili na maeneo yake ya kistratijia.
Sanusha Naidu ambaye ni mtaalamu wa Taasisi ya Mazungumzo ya Kimataifa yenye makao yake mjini Cape Town nchini Afrika Kusini anasema: "Afrika imekuwa medani ya ushindani wa kidiplomasia na masuala ya kistratijia wa madola makubwa yanayotaka kufikia malengo yao ya kimataifa. Russia na Marekani ni sehemu ya wanachama wa klabu ya nchi zinazoiona Afrika kuwa ndiyo njia ya kuimarisha satua na ushawishi wao kimataifa na kufikia malengo yao mapya."
Katika upande wa masuala ya kijeshi na kiusalama pia Afrika ina umuhimu mkubwa kwa Russia na tayari viongozi wa Moscow wameshafanya mazungumzo na wenzao wa nchi kadhaa Afrika kama Misri na Algeria kuhusu masuala ya kupambana na ugaidi hususan katika maeneo ya kaskazini mwa bara hilo, hali ya usalama na mivutano ya kisiasa nchini Libya na mikataba ya mauzo ya silaha kama ndege na helikopta za kivita, aina mbalimbali ya magari ya deraya na kadhalika.
Kwa kutilia maanani hayo yote tunaweza kusema kuwa, safari ya sasa ya Lavrov nchini Ethiopia ina umuhimu mkubwa zaidi katika pande mbili. Kwanza ni kwamba safari hiyo inayofanyika sambamba na ile ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika nchi kadhaa za Afrika ikiwemo Ethiopia yenyewe, ni kielelezo cha umuhimu wa nchi za Afrika na ushindani wa madola hayo mawili makubwa barani humo. Pili ni kwamba, safari hiyo ni katika jitihada za Russia za kutaka kupanua zaidi ushirikiano na nchi za bara hilo hususan katika masuala ya kiuchumi.