Marekani inakiuka haki za binadamu
Marekani imelaumiwa vikali kwa kukiuka haki za binadamu kitaifa na kimataifa.
Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, limetoa taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchni Marekani na kusema Washington inakiuka haki zinazotambuliwa kimataifa. Ripoti hiyo imebaini namna Wamarekani wenye asili ya Afrika wanavyouawa kiholela na polisi mbali na kuenea ubaguzi wa rangi nchini humo. Aidha ripoti hiyo imekosoa mfumo wa magareza Marekani na kusema nchi hiyo ina wafungwa takribani milioni 2.37,idadi ambayo ni kubwa zaidi duniani.
Ripoti hiyo imeashiria ubaguzi katika mfumo wa sheria Marekani na kusema katika hali ambayo kuna kiwango takribani sawa cha uhalifu unaohusu utumizi dawa za kulevya miongoni mwa Wazungu na Wamarekani Waafrika, lakini ni Wamarekani Waafrika ndio hukamatwa kwa wingi na kufungwa jela. Aidha ripoti hiyo imekosoa sera za Marekani za kuwapa mafunzo na silaha magaidi ambao inadaiwa wana misimamo ya wastani nchini Syria. Ripoti ya Human Rights Watch Pia imeikosoa Marekani kwa kutoa msaada na kushiriki katika hujuma za jeshi la Saudia nchini Yemen na kwa msingi huo Marekani imetajwa kuwa mshirika katika jinai na ukiukwaji wa sheria za vita nchini Yemen.