Kuarifishwa mgombea wa muungano wa wapinzani wa serikali nchini Kongo Brazzaville
Muungano mkuu wa vyama vya upinzani nchini Kongo Brazzaville umemtangaza mgombea atakayepeperusha bendera yake katika uchaguzi mkuu ujao nchini humo.
Muungano huo wa 'Union for Social Democracy' umemchagua Pascal Tsaty Mabiala kama mgombea wake katika uchaguzi huo. Uchaguzi mkuu nchini Kongo Brazzaville umepangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu. Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na akihutubia bunge la nchi hiyo, Rais Denis Sassou Nguesso wa Kongo Brazzaville alisisitiza kuwa, uchaguzi mkuu huo unapasa kufanyika katika miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu. Ni baada ya hapo ndipo tarehe 31 ya mwezi Disemba, serikali ya Brazzaville ikatangaza rasmi tarehe ya uchaguzi kuwa ni tarehe 20 mwezi Machi mwaka huu. Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi Julai. Chaguzi kuu zilizopita nchini Kongo Brazzaville zilifanyika mwezi Agosti mwaka 2002 na 2009. Christopher Willey, mchambuzi wa masuala ya Kiafrika anaelezea sababu ya kucheleweshwa kutajwa tarehe ya uchaguzi wa nchi hiyo kuwa inatokana na mpango wa viongozi wa chama tawala wa kutoa fursa kwa mgombea wake ili apate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi huo. Kwa mtazamo huo, viongozi wa chama tawala, wanakusudia kuwanyima wapinzani wa serikali fursa ya kutosha kwa ajili ya kuunda muungano wao wa kisiasa sanjari na kuainisha mgombea wake atakayepambana na Rais Denis Sassou Nguesso katika uchaguzi ujao. Hivi sasa vyama vya upinzani vina muda usiozidi kipindi cha miezi mitatu tu kwa ajili ya kuunda muungano, kumchagua mgombea na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi, katika hali ambayo kwa upande wake chama tawala hakina haja ya kufanya kampeni zaidi za kumtangaza Rais Sassou Nguesso kwa wapigakura. Mwaka jana rais huyo ambaye amekuwa akitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 31 kati ya 36 ya umri wake wa kisiasa, aliitisha kura ya maoni kwa ajili ya kukifanyia marekebisho kipengee cha katiba kinachohusu ukomo wa vipindi viwili vya uongozi. Licha ya kususiwa na vyama vya upinzani kura hiyo ya maoni, asilimia kubwa ya wapigakura walikubali kukifanyia marekebisho kipengee hicho na hivyo kutoa mwanya kwa rais huyo kuweza kushiriki kwa mara ya tatu katika uchaguzi ujao. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, ongezeko la uchumi lililoshuhudiwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na kadhalika kuimarika usalama na uthabiti wa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika, ni mambo yaliyoongeza uungaji mkono wa wananchi kwa Rais Denis Sassou Nguesso. Hata hivyo hatua ya muungano mkuu wa wapinzani ya kumtangaza mgombea wake katika uchaguzi, inatajwa kuwa muhimu sana ambayo inaweza kumfanya Rais Sassou Nguesso kushindwa katika uchaguzi huo. Muungano huo ambao ulisusia chaguzi za mwaka 2002 na 2009, sasa umeazimia kupambana vilivyo na chama tawala katika uchaguzi huo wa mwezi Machi. Pascal Tsaty Mabiala aliyechaguliwa na muungano huo wa upinzani dhidi ya serikali, tayari ametangaza vipaumbele vyake kwa ajili ya raia wa Kongo ambavyo ni pamoja na kuleta mshikamano na uadilifu wa kijamii. Aidha amesema kuwa, endapo atashinda katika uchaguzi ujao, basi atapambana na umasikini, ukosefu wa ajira na dhulma na kusisitiza kuwa, mambo hayo ndiyo yatakayopewa kipaumbele na serikali yake. Inaonekana wazi kwamba, Mabiala amefahamu kuwa hivi sasa raia wa Kongo Brazzaville wanataka kupunguzwa kiwango cha umasikini na ukosefu wa ajira nchini mwao, tatizo ambalo linawakabili zaidi vijana. Pascal Tsaty Mabiala alikuwa waziri wa ulinzi kati ya mwaka 1992-1997 yaani wakati wa utawala wa Pascal Lissouba, rais wa zamani wa nchi hiyo. Kwa sasa mwanasiasa huyo amekuwa mgombea wa nne kutangazwa kwa ajili ya kukabiliana na Rais Denis Sassou Nguesso katika uchaguzi wa tarehe 20 mwezi ujao. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, licha ya Rais Sassou Nguesso kufanikiwa kubadili kipengee cha katiba na hivyo kupata fursa ya kuweza kushiriki kwa muhula wa tatu katika uchaguzi ujao, lakini hatua ya vyama vya upinzani ya kuamua kutosusia uchaguzi huo, ni hatua muhimu inayoashiria kuwepo mpambano mkali katika uchaguzi.