Malengo ya safari ya Erdogan nchini Saudi Arabia
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameitembelea Saudi Arabia huku akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake. Akiwa katika hatua ya kwanza ya safari yake ya siku tatu katika nchi kadhaa za Ghuba ya Uajemi, Erdogan aliwasili Jeddah, Saudi Arabia Jumatatu Julai 17.
Mbali na maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Ankara, wafanyabiashara 200 wa Uturuki pia wameandamana na rais huyo katika safari hiyo ya siku tatu. Baada ya Saudi Arabia, ujumbe wa Uturuki umeelekea Qatar na UAE kwa utaratibu huo. Madhumuni halisi ya safari ya Rais Erdogan katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ni kuvutia uwekezaji kwa lengo la kujiondoa katika mgogoro wa kiuchumi unaoikabili Uturuki. Vyombo vya habari vya Uturuki vimetaja kuvutia uwekezaji wa dola bilioni 50 kutoka nchi tatu hizo za Kiarabu kuwa sababu kuu ya kufanyika safari hiyo. Kabla ya kuanza safari yake katika nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, Erdogan alisema anakusudia kupanua uhusiano na kukamilisha mikataba ya uwekezaji na nchi hizo.
Safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa Uturuki nchini Saudi Arabia inafanyika katika hali ambayo Uturuki inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Licha ya juhudi za viongozi wa Ankara, bei ya dola ya Marekani imeongezeka hadi kufikia lira 27 kwa dola, wakati kabla ya uchaguzi, serikali iliweza kuidhibiti kwenye mpaka wa lira 20. Licha ya uwepo wa misukosuko katika uhusiano wa Uturuki na nchi za Ghuba ya Uajemi hususan Saudi Arabia na Imarati hasa baada ya mapinduzi yaliyofeli ya mwezi Julai 2016 nchini Uturuki, inaonekana pande hizo zimeamua kupanua uhusiano wao ili kukidhi mahitaji yao. Uhusiano wa Uturuki na Saudi Arabia uliingia kijibaridi, hasa kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Saudia, katika ubalozi mdogo wa Saudia huko Istanbul. Kwa kadiri kwamba mahusiano ya kisiasa na kiuchumi ya nchi mbili yamepungua hadi kiwango cha chini kabisa.
Rais Erdogan kwanza alitaka kuhukumiwa wahusika wa jinai hiyo katika ardhi ya Uturuki. Lakini baada ya miaka minne, serikali yake ililazimika kukubali matakwa ya Saudi Arabia ili kuimarisha uhusiano wa pande mbili, ambapo la kwanza lilikuwa ni kufunga faili la kufuatiliwa mauaji ya Jamal Khashoggi katika ardhi ya Uturuki na kulikabidhi faili hilo kwa watawala wa Riyadh. Baada ya hapo Erdogan alipewa kibali cha kusafiri Saudi Arabia mwezi Aprili mwaka jana kwa lengo la kuzungumza na watawala wa Riyadh. Kwa kuzingatia propaganda za vyombo vya habari vya Uturuki, Saudi Arabia na nchi kadhaa za eneo, inaonekana kuwa Uturuki inazihitaji nchi za Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kutatua mgogoro wake wa kiuchumi.
Tathmini ya baadhi ya matukio inaonyesha kuwa Saudi Arabia, UAE na hata Qatar zinahitaji zaidi msaada wa Uturuki. Kwa uwekezaji mdogo tu nchini Uturuki, nchi hizo zitapokea mahitaji yao yote ya kijeshi kutoka Uturuki. Wakati huo huo uhusiano wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na Uturuki bado ni dhaifu na unaonekana kuendelea kuporomoka. Pamoja na hayo mahusiano ya muda yanayotokana na mahitaji ya muda mfupi yangali yanaendelea. Kwa mfano, vyombo vya habari vya Riyadh vilitangaza Januari mwaka jana kwamba viongozi wa Saudia walimfukuza nchini humo msomi mmoja wa chuo kikuu aliyeamua kumsifu Rais Erdogan.
Ingawa vyombo vya habari vya Riyadh havikufichua jina la mhadhiri huyo, lakini hatua hiyo ya serikali ya Saudia inathibitisha kuwa watawala wa nchi hiyo wako tayari kudumisha uhusiano wa pande mbili na Uturuki lakini kwa kiwango kinachoweza kudhibitika. Hii ni kwa sababu mgogoro wa kiuchumi wa Uturuki bado utaendelea kuwepo, na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ambazo hupata zaidi ya asilimia 90 ya mapatao yao kutokana na mauzo ya mafuta yasiyosafishwa, bado zitaendelea kuwa na uwezo wa kuidhibiti Uturuki kupitia ukiritimba wao katika uwanja huo. Wakati wa mazungumzo ya hivi karibuni na wajumbe wa Uturuki, hati 9 za makubaliano (MOU) zilitiwa saini kati ya pande mbili katika nyanja za nishati, mali isiyohamishika, ujenzi, elimu, teknolojia ya dijitali na afya.
Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia pia ilitangaza kutia saini mikataba kadhaa na kampuni ya Uturuki ya Baykar inayoengeneza ndege zisizo na rubani, hivyo inaonekana Saudi Arabia imefikia malengo yake katika safari ya Erdogan huko Riyadh. Hati hizo za makubaliano ya pande mbili zitachukua muda mrefu kabla ya kuanza kutekelezwa, kwa uchache miezi sita ijayo, ambapo kuna wakati wa kutosha kwa pande hizo kuzitathmini zaidi. Hakuna shaka kwamba Saudi Arabia, ikiwa ni nchi yenye rasilimali za nishati, hasa mafuta ghafi, inajaribu kujipatia nafasi salama katika eneo. Kinyume chake, Uturuki, ambayo haina rasilimali za nishati, ni kitovu cha matumizi na mauzo ya nishati katika eneo la Asia Magharibi, na hivyo inajaribu kupata itibari ya uaminifu duniani. Hili ni jambo ambalo haliwafurahishi sana watawala wa Saudia. Inaonekana kwamba watawala hao wametayarisha mipango kadhaa kwa ajili ya kuidhibiti Uturuki katika uwanja huo, mipango ambayo wataitekeleza wakati unaofaa.
Kwa ujumla ni kwamba, kwa mujibu wa habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya eneo, safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa Uturuki nchini Saudi Arabia imekuwa na manufaa zaidi kwa serikali ya Riyadh kuliko serikali ya Ankara. Hivyo tunaweza kusema kuwa serikali ya Ankara haijaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa kutokana na safari ya viongozi wake huko Saudi Arabia.