Upinzani Bahrain wapinga kuajiriwa madaktari wa Israel
(last modified Tue, 08 Aug 2023 07:22:41 GMT )
Aug 08, 2023 07:22 UTC
  • Upinzani Bahrain wapinga kuajiriwa madaktari wa Israel

Mrengo mkubwa zaidi wa upinzani Bahrain umekosoa vikali azma ya utawala wa Aal-Khalifa ya kuwaajiri madaktari wa utawala haramu wa Israel katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Jumuiya ya Kitaifa na Kiislamu nchini Bahrain ya Al-Wifaq imesema ni jambo lisiloingia akilini kwa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu kutaka kuwaajiri madaktari wa Kizayuni katika hali ambayo nchi mbili hizo za Kiarabu zina mamia ya madaktari wanaosaka ajira.

Kwa mujibu wa Al-Wifaq, utawala wa Aal-Khalifa unapanga kuwapa madaktari hao wa Israel mshahara mara tatu zaidi ya kiwango cha kawaida, elimu ya bure kwa watoto wao, 'viza ya dhahabu' itakayowaruhusu kuishi nchini humo kwa muda mrefu pamoja na manufaa mengine.

Kundi hilo kubwa zaidi la upinzani lenye mielekeo ya Kiislamu nchini Bahrain limesema mpango huo wa kuajiriwa madaktari wa Kizayuni ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na utawala wa Aal-Khalifa za kuimarisha uhusiano na utawala ghasibu wa Kizayuni na kulifanya kuwa suala kawaida.

Wabahrain wanapinga uhusiano wa kawaida na Isreal

Mapema mwaka huu, wanazuoni wa Bahrain walikosoa vikali pia mpango wa Aal-Khalifa wa kuwauzia ardhi Wayahudi wakisisitiza kuwa, kitendo hicho ni sawa na kuiuza nchi na ni haramu.

Septemba 2020, viongozi wa Bahrain na wa utawala haramu wa Israel walisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mbele ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Bahrain na utawala haramu wa Israel, duru za habari ziliripoti mpango wa kutengwa eneo maalumu la Mayahudi katika mji mkuu wa nchi hiyo Manama.