Wapinzani Wazayuni "wala sahani moja" na Netanyahu mjini New York
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i102510-wapinzani_wazayuni_wala_sahani_moja_na_netanyahu_mjini_new_york
Kama ilivyokuwa imetabiriwa tangu zamani, safari ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu ya kushiriki kwenye mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New Yoirk Marekani, imekuwa na vioja vingi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 21, 2023 23:10 UTC
  • Wapinzani Wazayuni

Kama ilivyokuwa imetabiriwa tangu zamani, safari ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu ya kushiriki kwenye mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New Yoirk Marekani, imekuwa na vioja vingi.

Wapinzani wa nduli huyo Mzayuni ndani ya utawala wa Kizayuni wamemwandama muda wote kwa viroja na vitimbi vingi katika miji tofauti ya Marekani kiasi kwamba, kila sehemu ambayo Netanyahu alipanga kuitembelea, ameandamwa kwa matusi na kejeli kutoka kwa wapinzani wa ndani ya Israel. 

Mkusanyiko wa kwanza wa wapinzaji wa Netanyahu umefanyika mbele ya hoteli aliyofikia katika upande wa mashriki wa Manhattan na baada ya hapo wamemwandama kama kivuli popote alipoenda. Elon Reeve Musk, mmiliki wa shirika la Tesla na SpaceX (Twitter ya zamani) wakati alipoonana na Netanyahu, mazungumzo ambayo yamepingwa vikali na wapinzani wa waziri mkuu huyo wa Israel amesema, hadi hivi sasa haijapata kutokea mfanyakazi yoyote wa Tesla kupinga maamuzi yake kama ilivyotokea wakati huu nilipoamua kuzungumza na Netanyahu.

Baada ya kukumbwa na upinzani huo mkubwa, Netanyahu alilazimika kubadilisha lugha kuhusu sheria ya kufanyia marekebisho mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni. Wapizani wake wanasema mabadiliko hayo ni kufanya mapinduzi dhidi ya mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni. Netanyahu amepunguza kidogo makali ya matamshi yake katika kutetea marekebisho hayo ambapo wachambuzi wa mambo wanasema ni njama binafsi tu za  Netanyahu, kujipunguzia mashinikizo.

Wapinzani wa Netanyahu katika maandamano ya kumlaani waziri mkuu huyo wa Israel nchini Marekani

 

Katika mazungumzo yake na Elon Musk, Netanyahu amekiri kuwa, marekebisho ya mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni si ya kiadilifu na hayana mlingano sawa, lakini wakati huo huo amesema, wapinzani wake ni wajinga na wapumbavu. Amesema, wengi wa wapinzani wake hata hawajui chochote kuhusu istilahi za kisheria zinazotumika kwenye marekebisho hayo.

Vilevile ameishutumu mahakama kuu ya Israel kuwa inadhibitishwa na kijikundi kidogo cha watu na kudai kwamba, sisi tunataka mahakama hiyo iwe mali ya watu si kikundi kidogo cha watu. 

Matukio ya miezi kadhaa ndani ya utawala wa Kizayuni yanaonesha kuwa, Netanyahu na genge lake lenye misimamo mikali ya kulia, hawajawahi kulegeza misimamo hata mara moja isipokuwa tu pale wanapoona mashinikizo yamekuwa makubwa na uwepo wa utawala pandikizi wa Israel umo hatarini. Wamapohisi hivyo ndipo huwa wanajifanya kulegeza misimamo ili kujipunguzia mashinikizo.

Muswada wa marekebisho ya mfumo wa mahakama ya Israel ambayo kimsingi yamependekezwa na kusimamiwa kikamilifu na waziri wa mahakama wa utawala wa Kizayuni, Yariv Levin, ulikuwa ajenda kuu ya serikali ya Netanyahu tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi mwezi Machi. Muswada huo una nia ya kuwakingia kifua viongozi wa utawala wa Kizayuni ili wasifuatiliwe kisheria hata wanapofanya ufisadi mkubwa kama aliofanya Netanyahu na familia yake. Hadi tarehe 27 Machi 2023 muswada huo ulikuwa ndiyo ajenda kuu ya baraza la mawaziri la Netanyahu. Lakini serikali hiyo ililazimika kulegeza kamba na kuuondoa muswada huo kwenye ajenda zake kuu kutokana na upinzani mkali na baada ya kufutwa kazi waziri wa vita wa Israel, Yoav Gallant. 

Benjamin Netanyahu

 

Miezi iliyofuata upinzani dhidi ya muswada huo umeongezeka na kila wiki mamia ya maelfu ya wakazi wa utawala wa Kizayuni wanafanya maandamano dhidi ya Netanyahu. Pamoja na hayo Netanyahu na genge lake lenye misimamo mikali ya kulia huko Israel wanaendelea kushikilia misimamo yao ya kutaka bunge la utawala wa Kizayuni liwe na nguvu za kudhibiti idara ya mahakama ya utawala huo, ili Netanyahu na familia yake wawe katika amani na wasifuatiliwe tena na mahakama katika tuhuma kubwa za ufisadi zinazowaandamana.

Baada ya serikali ya Netanyahu kulazimika kuutoa muswada wa marekebisho ya mahakama katika ajenda zake kuu tarehe 27 Machi, 2023, imelazimika pia kulegeza misimamo na kuamua kupasisha kifungu kimoja kimoja cha muswada huo licha ya kwamba kila kipengee kinachopasishwa kinakumbwa na upinzani mkali wa Wazayuni. Hadi hivi sasa vifungu viwili vya muswada huo vimepasishwa kwa nyakati tofauti, kimoja ni cha sheria ya kuuzuliwa waziri mkuu na kingine ni cha sheria ya kufuta "maamuzi yanayoingia akilini" maarufu kwa jina la "reasonableness doctrine."

Vifungu vyote hivyo viwili vimepasishwa kwa jina la marekebisho makuu ya kimsingi ya sheria kwa maaana ya kwamba idara ya mahakama ya Israel haina uthubutu wa kubatilisha marekebisho hayo. Kwa mujibu wa marekebisho hayo, hivi sasa idara ya mahakama ya Israel haina uwezo tena wa kumfuta kazi waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Kiujumla ni kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa unapitia kipindi kigumu sana cha migogoro ya ndani na nje. Maandamano ya kila wiki yanafanyika kwenye ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, na popote wanapokwenda viongozi wa utawala wa Kizayuni akiwemo waziri mkuu mwenye misimamo mikali ya Kizayuni yaani Benjamin Netanyahu wanaandamwa kama kivuli na wapinzani wao.